Mashabiki wakosa kuamini huku Snoop Dogg akitangaza kuacha bangi baada ya kuivuta kwa miaka mingi

Snoop Dogg anajulikana kuwa mpenzi mkubwa wa bangi na amekuwa hafichi hilo kwa miaka mingi.

Muhtasari

•Snoop Dogg alitangaza ameamua kuachana na mihadarati hiyo baada ya kufikiria sana na kushiriki mazungumzo mengi na familia yake.

•Snoop Dogg ni mpenzi mkubwa wa mihadarati hiyo na inaripotiwa kuwa anafanya biashara inayohusisha bidhaa za bangi. 

Image: INSTAGRAM// SNOOP DOGG

Rapa maarufu wa Marekani Calvin Broadus almaarufu Snoop Dogg aliwaacha maelfu ya mashabiki katika hali ya kutoamini baada ya kutoa tangazo la kushangaza kwamba ameamua kuacha kuvuta bangi.

Snopp Dogg, ambaye amekuwa kwenye tasnia ya burudani kwa takriban miongo mitatu iliyopita anajulikana sana kuwa mpenzi mkubwa wa bangi na amekuwa hafichi hilo kwa miaka mingi.

Siku ya Alhamisi hata hivyo, alitangaza kwamba ameamua kuachana na mihadarati hiyo baada ya kufikiria sana na kushiriki mazungumzo mengi na familia yake.

"Baada ya kufikiria sana na mazungumzo na familia yangu, nimeamua kuacha kuvuta bangi," Snoop Dogg aliandika kwenye kurasa zake za mtandao wa kijamii.

Aliambatanisha tangazo lake na picha yake akiwa ameshikilia mikono yake mbele ya uso wake, ishara inayotumika sana kuashiria unyenyekevu.

Rapa huyo mwenye umri wa miaka 52 hata hivyo hakushiriki maelezo zaidi kuhusu uamuzi wake au kufichua kama kuna suala la kiafya lililosababisha uamuzi huo.

"Tafadhali mheshimu faragha yangu kwa wakati huu," aliomba.

Snoop Dogg ni mpenzi mkubwa anayejulikana wa mihadarati hiyo ambayo ni haramu nchini Kenya na inaripotiwa kuwa anafanya biashara inayohusisha bidhaa za bangi. Kumekuwa na ripoti zilizopita kuwa rapa huyo mwenye umri wa miaka 52 alianza kuuza mihadarati hiyo akiwa bado shuleni.

Mashabiki ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa miaka mingi walikuwa na maoni mseto kuhusu habari hizo, huku baadhi yao wakiwa hawaamini na wakifanya mzaha kuhusu uamuzi wa ghafla wa Snoop Dogg.

Tazama maoni ya baadhi ya mashabiki;

Cianacurry: Ninaheshimu uamuzi wake sana, lakini hiki ndicho kitu cha kuchekesha zaidi ambacho nimewahi kuona. Nitakumbuka hii milele.

Mvalles: Dunia inaisha kweli.

Mbs505: Snoop Mpya hakika atavutia.

Lukas09_: Mtu alidukua simu ya Snoop.

Mmfgreen: Nadhani sote tunajua jinsi 'nimeacha' itaisha.