Msanii wa injili Guardian Angel amefunguka kuhusu mitazamo yenye utata na mwanablogu Andrew Kibe, haswa kuhusu watu maarufu wa Kenya na maisha yao ya kifamilia na yale ya kibinafsi.
Angel katika mahojiano na blogu ya Plug TV, alisema kwamba yeye hawezi kutishwa wala kuchukulia maanani kauli za Andrew Kibe haswa katika masuala yanayolenga familia yake na mpenzi wake Esther Musila.
Msanii huyo ambaye hivi majuzi alizindua lebo yake ya muziki, Seven Heaven Music, alisema bila kupepesa jicho kwamba kauli za Kibe zinaonesha moja kwa moja mtu ambaye amevamiwa na mapepo ya kishetani.
Kwa mujibu wa Guradian Angel, Kibe anasumbuliwa na mapepo kwa vile aliacha Imani na kuanza kujihusisha na mambo ya kidunia mpaka wakati mmoja akakiri wazi kwamba hana Imani kuhusu uwepo wa Mungu.
"Unajua alikuwa ameokoka, kwa hiyo ni nini kilimtokea aliporudi nyuma? Kwa hiyo sasa hivi ukianza kugombana naye ujue unagombana na mtu aliyekaliwa na ibilisi mara saba zaidi ya alivyokuwa kabla hajateleza na kurudi nyuma," alisema.
Angel alimsuta Kibe kwa kuendelea kutoa maneno na kauli kwamba uhusiano wake na Esther Musila hautakuwa wa kudumu kutokana na upana wa umri baina yao.
Angel ana miaka 33 huku Musila akiwa na takriban miaka 53.
"Hujaoa mwanamke mzee kama mimi, lakini uko sawa huko uliko? Unajua, tumefanya miaka miwili, na kuna watu wengi ambao walidhani hatutaweza, walisema hatutadumu, walikuwa kwenye ndoa zao na sasa wameachana na wenza wao, wengine hata wamekufa. Mambo mengi yanaweza kutokea ndani ya miaka miwili,” alisema huku akicheka.