Kwa nini shughuli ya kuchangisha pesa mtandaoni kwa matibabu ya Mwana Mtule ilisitishwa na KNH

Wasanii walikuwa wamejaribu kumchangishia pesa Mwana Mtule mtandaoni lakini usimamizi wa KNH ukazuiwa.

Muhtasari

• 2mbili alijaribu kufanya uchangishaji mtandaoni kwa ajili ya bili ya hospitali ya  Mwana Mtule lakini kipindi hicho hakikuweza kuendelea.

•Kipindi hicho kilikatishwa na ofisa wa hospitali hiyo ambaye aliwataka waache kurekodi video kwa sababu hairuhusiwi hospitalini.

akiwa amelazwa KNH.
Mwanamuziki Mwana Mtule akiwa amelazwa KNH.
Image: INSTAGRAM//2MBILI

Siku ya Jumamosi jioni, mchekeshaji 2mbili alijaribu kufanya uchangishaji mtandaoni kwa ajili ya bili ya hospitali ya  mwanamuziki Mwana Mtule lakini kwa bahati mbaya kipindi hicho hakikuweza kuendelea kama ilivyokusudiwa.

2mbili alikuwa ametangaza awali kuwa angefanya kipindi cha moja kwa moja kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kutoka Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, wodi 10B ambapo mwimbaji huyo wa nyimbo za injili ambaye ni mgonjwa amelazwa kwa sasa katika juhudi za kukusanya pesa za bili ya hospitali ambayo sasa imepanda hadi karibu shilingi nusu milioni.

"Habari za familia, nitakuwa nikipeperusha moja kwa moja kwenye mitandao yangu ya kijamii kuanzia saa kumi na moja jioni katika Wadi ya 10B ya KNH ili kuchangisha bili ya matibabu ya Mwana Mtule ambayo sasa ni 400k plus!!" 2mbili aliandika kwenye Instastori zake.

Aliongeza, “Pesa zitatumwa moja kwa moja kwenye Paybill yake: 891300, Acc. Nambari: 82998."

Kwa kweli, Jumamosi jioni kipindi hicho cha moja kwa moja kilianza kama ilivyotangazwa awali kabla ya kukatishwa na ofisa wa hospitali hiyo ambaye aliwataka waache kurekodi video kwa sababu hairuhusiwi hospitalini.

“Samahani jamani, tulilazimika kumaliza kipindi cha moja kwa moja kwa sababu ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa uongozi wa knh!!! Asanteni kwa mchango,” 2mbili aliandika kwenye taarifa.

Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha afisa wa hospitali akimweleza mchekeshaji huyo kwamba kurekodi video na picha katika KNH hairuhusiwi.

2mbili aliyekuwa akiendesha harambee hiyo ya mtandaoni alionekana akijadiliana na afisa huyo wa kike akimtaka awaruhusu kufunga kipindi cha kuchangisha fedha.

“Sawa, tumekiuka sheria. Ila inabidi utulie tuambie mgonjwa tunaenda. Hatukai sehemu moja sote, tunapaswa kuagana. Hata tuko na mchungaji pale. Huyo ni mchungaji mzima lazima aombee mgonjwa tukienda,” 2mbili alisikika akimwambia afisa huyo.

Afisa huyo alimweleza kuwa tayari alikuwa amemjulisha mke wa Mwana Mtule kuhusu sheria ambayo hairuhusu kupiga picha hospitalini.

Stevo Simple Boy ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao walikuwa wamejitokeza katika hospitali ya KNH wakati wa kipindi hicho cha moja kwa moja ili kumuunga mkono mwanamuziki mwenzake ambaye amekuwa akiugua kwa wiki kadhaa.