logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Nyako alia kwi kwi baada ya akaunti ya benki ya mapato kutoka TikTok kufungwa

“Akaunti yangu ya benki imefungwa. Siwezi kuipata. Imezuiwa." Nyako alilia.

image
na Davis Ojiambo

Burudani04 December 2023 - 07:10

Muhtasari


  • • Nyako alifichua kwamba huenda watu wanaomhangaisha wakati anajaribu kujipatia riziki kupitia TikTok ndio wale wale ambao walimvurugia kibarua chake siku za nyuma.
Nyako.

TikToker wa Kenya mwenye makazi yake nchini Ujerumani, Rose Atieno maarufu kama Nyako amelia akidai kwamba hajui ni nani amefanya nini kupelekea akaunti yake ya benki anayotumia kupokea mapato kutoka kwa mitikasi yake ya TikTok kufungwa.

Katika video moja ambayo imekuwa ikienea mitandaoni wikendi iliyopita, Nyako alionekana mwenye majonzi akieleza kwa huruma kwamba hajui ni nini kilitokea kwani ameshindwa kabisa kufikia akaunti yake ili kufanya miamala ya kulipia bili zinazomkodolea macho.

Alihisi kwamba pengine kuna mtu amemripoti kwa serikali kupitia mamlaka ya ukusanyaji ushuru kutokana na kipato kikubwa ambacho anakitengeneza kutoka TikTok pasi na kulipia ushuru.

“Akaunti yangu ya benki imefungwa. Siwezi kuipata. Imezuiwa. Sijui nani aliandika nini tena kwa serikali wakati huu. Lazima nilipe kodi yangu kutoka TikTok. Lazima nilipe bima yangu kutoka kwa TikTok. Pesa hizo zimechukuliwa. Sijui hata nianzie wapi wakati huu. Sijui nimuulize nini,” alisema.

Nyako alifichua kwamba huenda watu wanaomhangaisha wakati anajaribu kujipatia riziki kupitia TikTok ndio wale wale ambao walimvurugia kibarua chake siku za nyuma.

“Watu walewale walionifanya nipoteze kazi. Nilikuwa naenda kazini. Nilikuwa naamka asubuhi na mapema sana kama kila mtu mwingine na kwenda kazini. Niliridhika sana na kufurahishwa na kazi yangu hadi watu wale wale kwenye TikTok walikusanyika ili kuninyima haki ya kwenda kazini. Mtu aliniandikia barua mahali pa kazi. Na nilipoteza kazi ndani ya saa 24,” alisema.

Hii inakuja siku chache baada ya kupapurana na mjasiriamali Akothee kuhusu nani anayemuiga nani kati yao katika mtandao huo wa video fupi.

Akothee alikuwa wa kwanza kuathirika na majibizano yao baada ya TikTok kuifunga kwa muda akaunti yake kabla ya Nyako naye kuja na dai kwamba akaunti ya benki inayohusika kupokea mapato ya TikTok nayo imefungwa vile vile.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved