Rozzie afunguka kwa nini familia ya Lebanon aliyokuwa akifanyia kazi ililia alipokuwa akiondoka

Rozzie aifichua kuwa amerejea Kenya kwa likizo kisha anapanga kurejea Lebanon.

Muhtasari

•Rozzie amefunguka kuhusu video inayosambaa ya kipindi cha kihisia wakati akiaga familia ambayo amekuwa akiifanyia kazi nchini Lebanon.

•Rozzie alikanusha madai kwamba watoto aliokuwa akiwatunza walikuwa karibu sana naye kwani mwajiri wake alikuwa amewatelekeza.

akiondoka Lebanon
Rozzie akiondoka Lebanon
Image: HISANI

Mwanadada wa Kenya ambaye amekuwa akivuma kwenye mitandao ya kijamii, Roseline Atieno almaarufu ‘Rozzie’ amefunguka kuhusu video inayosambaa ya kipindi cha kihisia wakati akiaga familia ambayo amekuwa akiifanyia kazi nchini Lebanon.

Katika siku kadhaa zilizopita, video inayoonyesha nyakati zenye hisia kali wakati Rozzie, wanandoa aliokuwa akiwafanyia kazi na watoto wao wanne wakiagana imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakionekana kuguswa sana na upendo ulioonyeshwa.

Katika mahojiano na Bennie Experience, mama huyo wa watoto watatu alieleza zaidi kuhusu upendo mwingi kati yake na watoto aliokuwa akiwatunza.

"Nadhani ni upendo wa mama tu ambao nimekuwa nikiwapa kwa sababu pia nina watoto. Nilikuwa nikiwachukulia kama watoto wangu tu,” Rozzie alisema.

Wakati uo huo, mwanamke huyo anayetoka Kaunti ya Siaya alikanusha madai kwamba watoto aliokuwa akiwatunza walikuwa karibu sana naye kwani mwajiri wake alikuwa amewatelekeza.

"Sio kweli, alikuwa kila wakati kwa watoto wake," alisema.

Rozzie alisema kwamba alifahamu kuhusu video yake inayovuma kutoka kwa rafiki yake anayeishi Lebanon baada ya kuwa tayari imeanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

"Nilifurahia .. familia ya Lebanon ilikuwa na furaha kwangu," alisema.

Akizungumzia kazi yake nchini Lebanon, alifichua kwamba aliondoka Kenya kuelekea hiyo  ya Mashariki ya Kati mnamo 2021 ili kutafuta pesa za kumsaidia kuwatunza watoto wake wawili.

Alifichua kuwa amerejea Kenya kwa likizo kisha anapanga kurejea Lebanon.

"Nitarudi.. nikipewa kazi nchini Kenya nitafanya kazi," alisema.

Mama huyo wa watoto watatu pia alisema anafurahi kuona wasaidizi wa nyumbani wengine wa Kenya wakishughulikiwa vyema baada ya video yake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.