Rozzie afunguka sababu ya kuiaga familia ya Lebanon iliyomlilia alipokuwa akiondoka

Rozzie alitaja kipindi kile cha kihisia kabla ya kuondoka Lebanon kama wakati wa huzuni zaidi maishani mwake.

Muhtasari

•Rozzie alitaja kipindi hicho cha kihisia kabla ya kuondoka Lebanon kama wakati wa huzuni zaidi maishani mwake.

•Mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa amerejea nchini Kenya kwa likizo kisha anapanga kurejea Lebanon.

Bi Roseline Akinyi almaarufu Rosie
Image: HISANI

Bi Roseline Atieno Oyola almaarufu Rozzie, mwanamke wa Kenya ambaye amekuwa akivuma kwenye mitandao ya kijamii katika siku chache zilizopita baada ya video yake yenye hisia kali akiaga familia ya Lebanon ambayo amekuwa akifanya kazi kwa miaka miwili iliyopita amesema kipindi hicho kwenye uwanja wa ndege kilimpata na hisia mseto.

Katika mahojiano na Presenter Ali, mama huyo wa watoto watatu alitaja kipindi kile cha kihisia kabla ya kuondoka Lebanon kama wakati wa huzuni zaidi maishani mwake.

Alisema alijisikia vibaya sana kuwaacha wanandoa ambao amekuwa akiwafanyia kazi tangu Oktoba 2021 pamoja na watoto wao wanne wadogo ambao amekuwa akiwatunza.

"Ilikuwa wakati wa huzuni zaidi maishani mwangu. Ilijawa na hisia tofauti kwa sababu kwa upande mmoja nilifurahi kuja kukutana na familia yangu na kwa upande mwingine nilikuwa na huzuni kwa sababu nilikuwa naacha watoto ambao nimeishi nao kwa miaka miwili,” Rozzie alisema.

Mwanamke huyo anayetoka Bondo katika Kaunti ya Siaya pia alifunguka kuhusu uhusiano mzuri na muungano thabiti kati yake na watoto wa mwajiri wake.

Alisema alijisikia kukaribishwa sana alipokuwa na familia ya Lebanon kwani wote walimtendea vyema na walithamini kazi nzuri aliyowafanyia.

“Hapo nilijisikia kuwa nyumbani. Tofauti pekee ni mimi nilikuwa nalipwa. Ninawapenda watoto kwa sababu wanathamini kazi yangu na wananipenda kwa hilo. Walikuwa wakinichukulia kama mzazi wao,” alisema.

Akizungumzia jinsi alivyojipata akifanya kazi kwa familia ya Lebanon, Rozzie alifichua kwamba aliondoka Kenya kuelekea Lebanon miaka miwili iliyopita kutafuta riziki bora.

"Nilikuwa nikiomba nipate boma yenye watu wenye moyo mwema na kwa bahati Mungu alijibu maombi yangu," alisema.

Rozzie alisema kwamba alipofika Lebanon na kukaribishwa na mwajiri wake, aliingiana vizuri na familia hiyo mara moja na walikuwa na uhusiano mzuri hadi alipoondoka.

Kuhusu ni kwa nini aliondoka Kenya kutafuta kazi, alisema alihitaji kutafuta njia za kuwahudumia watoto wake kwani ndoa yake ilikuwa imevunjika.

"Nilikuwa kwenye ndoa na baada ya kutofaulu, niliamua kwenda kutafuta malisho ya kijani ili kuleta utulivu wa maisha ya watoto wangu," alisema.

Katika mahojiano na Bennie Experience, Rozzie alifichua kuwa amerejea Kenya kwa likizo kisha anapanga kurejea Lebanon.

"Nitarudi.. nikipewa kazi nchini Kenya nitafanya kazi," alisema.