Expeditions Maasai Safaris yajishindia tuzo ya kifahari baada ya kumtambua Nanny Rosie

Kampuni hiyo ilitambuliwa kama Chapa bora ya Utalii na Usafiri ya Kenya katika hafla ya tuzo ya Top Star

Muhtasari

•Expeditions Maasai Safaris, imetambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya Utalii katika Tuzo za Mwaka huu za Top Star Brands.

•Bw Pancras Karema alibainisha kuwa uaminifu na uungwaji mkono wa wateja wao ndio umewashindia zawadi hiyo.

akimtuza Roseline Atieno.
CEO wa Expeditions Safaris Bw Pancras Karema akimtuza Roseline Atieno.
Image: EXPEDITIONS SAFARIS

Kampuni maarufu ya utalii ya Kenya, Expeditions Maasai Safaris, imetambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya Utalii na Usafiri nchini katika Tuzo za Mwaka huu za Top Star Brands.

Kampuni hiyo ambayo inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji Pancras Karema mnamo Ijumaa jioni ilitambuliwa kama Chapa bora ya Utalii na Usafiri ya Kenya katika hafla ya tuzo ya Top Star iliyofanyika katika Hoteli ya Sarova Panafric.

Wakati akisherehekea ushindi huo, Bw Pancras Karema alibainisha kuwa uaminifu na uungwaji mkono wa wateja wao ndio umewashindia zawadi hiyo.

"Tunatoa tuzo hii kwa wateja na wafuasi wetu wote waaminifu na tunaahidi kuendelea kuwapa huduma bora zaidi ya likizo," Bw Karema alisema.

Mkurugenzi mkuu, Bw Lawrence Ndegwa alichukua fursa hiyo kuwahakikishia wateja wao kuhusu kujitolea kwao katika kutoa huduma bora ya utalii.

"Utambuzi huu pia unatukumbusha matarajio makubwa ambayo wateja wetu wanayo kama chapa bora ya usafiri ya Kenya. Tunasalia kujitolea kutimiza matarajio haya na tunaboresha kila mara ili kutoa thamani kwa wateja wetu wote waaminifu," Ndegwa alisema.

Kufuatia mafanikio hayo, kampuni hiyo maarufu pia imesisitiza kujitolea kwake katika kuinua viwango vya sekta ya usafiri na utalii.

Kampuni ya Expeditions Maasai Safaris imejishindia tuzo hiyo siku chache tu baada ya kumtambua mwanadada wa Kenya Roseline Atieno almaarufu Nanny Rosie ambaye amekuwa akivuma kwenye mitandao ya kijamii baada ya video yenye hisia kali akiaga familia ya Lebanon ambayo amekuwa akiifanyia kazi kuwagusa moyo watumiaji wengi wa mtandao.

Kufuatia kujitolea ambako Rosie aliionyesha kwa kazi yake nchini Lebanon, kampuni ya Expeditions Maasai Safaris mapema wiki hii ilimsherehekea kwa kumpa likizo ya bure katika mbuga kubwa la Masai Mara ili kusherehekea na familia yake.

"Tuliguswa moyo sana na hadithi ya Rozah na uhusiano wake wa ajabu na familia anayoitumikia Lebanon. Kujitolea na upendo wake unajumuisha roho ya huruma tunayothamini katika Safari za Safari za Maasai," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Expeditions Maasai Safaris, Bw Pancras Karema wakati akimtunza Rosie mapema wiki hii. .

Kampuni hiyo ilimpa Rosie na familia yake safari hiyo ili waweze kuzama katika turathi tajiri za kitamaduni za Kenya, wanyamapori wa aina mbalimbali na mandhari nzuri, na kuhakikisha tukio lisilosahaulika.