Tamasha la gwiji wa Rhumba kutokea DRC, Koffi Olomide lilikuwa la kufana na lilihudhuriwa na watu wenye haiba na kutoka matabaka mbali mbali.
Miongoni mwa watu waliofurahia kushiriki nafasi adimu ya kutumbiziwa moja kwa moja jukwaani na Koffi Olomide ni mwanasiasa George Wajackoyah lakini pia watangazaji wa Radio Jambo, ambyo ilikuwa ni moja ya stesheni mfadhili wa tamasha hilo.
Katika video, mtanazaji Gidi wa kipindi cha Patanisho alionekana mwenye bashasha ghaya jukwaani akicheza densi nyuma ya Koffi Olomide kwa furaha.
Gidi, ambaye ni shabiki shakiki wa Arsenal alikuwa amevalia jezi ya njano ya timu hiyo huku muu mmoja akiwa amekunja suruali ndefu tayari kulisakata densi.
Alipakia picha hizo pamoja na video na kumshukuru Koffi Olomide kwa nafasi adimu ya kushiriki jukwaa na yeye huku akimsifia kwa mchango wake mkubwa kwa miongo mingi katika tasnia ya muziki wa Afrika.
“Asante LEGEND Koffi Olomide kwa kumbukumbu, mchango wako katika muziki wa Kiafrika ni hadithi nzuri ya kusimuliwa,” alisema.
Kwa upande wake, mtangazaji mwenza, Ghost alipakia video wakishiriki densi ya taratibu awali kabla ya ujio wa Koffi kwenye jukwaa.
Ghost katika video hiyo walicheza na Gidi kwa nyimbo taratibu za bendi ya Les Wanyika ambao walitumbuiza awali kumkaribisha Koffi Olimide jukwaani.
Koffi Olomide aliwapunga wengi alipotua jukwaani kwa mbwembwe zake za ujana, japo ni mtu mzima na umri wa kutukuka.
Wengi walibaki vinywa wazi wakizungumzia minenguo yake laini lakini pia fasheni yake, kwani alionekana amevalia viatu vyenye visigino virefu vinavyohusishwa na wanawake.