Mwanahabari mashuhuri wa kimataifa wa Kenya Larry Madowo amelalamikia hitilafu za umeme za mara kwa mara ambazo zinaathiri uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa nchini Kenya, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta almaarufu JKIA.
Madowo ni miongoni mwa Wakenya na watalii wengi waliokuwa katika JKIA Jumapili usiku wakati uwanja huo wa ndege ulipokumbwa na giza kubwa.
Huku akilalamika kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, mwanahabari huyo wa CNN alisema kuwa umeme ulipotea katika uwanja wa ndege mara tatu alipokuwa akisubiri ndege yake.
“Nilikumbana na kukatika kwa umeme mara tatu katika JKIA nilipokuwa nikisubiri ndege yangu. Tutaambia nini watu,” Larry Madowo alisema kwenye Facebook.
Alishare video na picha zinazoonyesha giza kubwa lililokuwa limekumba uwanja huo wa ndege wa kimataifa.
Mtangazaji huyo wa zamani wa NTV alisema katika nchi nyingi alizopitia duniani, ni Kenya pekee ambapo ameona umeme ukipotea katika uwanja wa ndege wa kimataifa.
“Kumekuwa na hitilafu tatu za umeme JKIA tangu nilipofika hapa saa moja iliyopita. Ninapitia takriban viwanja 50 vya ndege vya kimataifa kwa mwaka. Huu ndio pekee ambao nimeona ukipoteza umeme, na mara kwa mara," alisema.
JKIA ilikuwa miongoni mwa maeneo mengi ya nchi ya Kenya ambayo yaliathiriwa na kukatizwa kwa umeme kwa wingi mnamo Jumapili jioni.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) katika taarifa yake ya Jumapili jioni iliomba radhi kwa mteja walioathiriwa na tatizo la hivi punde lililoathiri Terminal 1A na 1E.
Walieleza kuwa giza kwenye vituo hivyo viwili lilitokana na kushindwa kwa jenereta zinazopaswa kusambaza umeme pale baada ya kupotea kwa stima.
"Tungependa kuwahakikishia umma kwamba sehemu nyingine ya uwanja wa ndege, ikiwa ni pamoja na JKIA Tower na Runway, iliendelea kufanya kazi kikamilifu na haikuathiriwa na tukio hili," KAA ilisema.
Mamlaka hiyo pia ilithibitisha kuwa mafundi wao waliweza kurekebisha tatizo la jenereta na umeme ulirejea katika vituo vilivyoathirika kwa muda mfupi.
"Katika dhamira yetu ya ubora wa huduma na kutegemewa kiutendaji, tumeanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini sababu kuu ya kuharibika kwa jenereta," walisema.