Muigizaji na mtayarishaji wa maudhui maarufu wa Kenya Caroline Muthoni Ngethe almaarufu Carrol Sonnie ana bahati sana kuwa hai leo baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani.
Katika taarifa yake ya Alhamisi jioni, mpenzi huyo wa zamani wa mchekesaji Mulamwah alifichua kwamba yeye miongoni mwa wengine ambao hakuwataja nusura wapoteze maisha yao katika ajali mbaya ya barabarani..
Sonnie alisema hata kama walitoka kwenye ajali hiyo wakiwa hai, tukio hilo la kuogofya lilimuacha akiwa na hofu na kiwewe.
"Aki Mungu. Karibu tupoteze maisha yetu katika ajali ya gari.. Mungu wetu ni Mungu wa nafasi nyingine," Carrol Sonnie alisema kupitia Instastories yake.
Aliongeza, "Nimeingiwa na kiwewe sana. Ee mungu!"
Mama huyo wa binti mmoja hata hivyo hakufichua maelezo mengine zaidi kuhusu ajali hiyo ya kutisha. Hata hivyo aliendelea kutoa shukrani zake kwa Mungu kwa kumuokoa kutokana na tukio hilo la kutisha.
Muigizaji huyo na mzazi mwenzake Mulamwah takriban miezi miwili iliyopita walijibizana hadharani kuhusu suala la ushirikiano katika malezi ya binti yao wa miaka miwili.
Mnamo mwezi Oktoba, Mulamwah alileza nia yake ya kusaidia katika malezi ya mtoto wake wa pekee na Carrol Sonnie.
Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, baba huyo wa mtoto mmoja hata hivyo alidai kwamba haijakuwa rahisi kwake kuhusika katika maisha ya bintiye.
Alidai kuwa kila anapotuma pesa au zawadi za kumtunza binti huyo wake wa miaka miwili, hurejeshwa kwake.
"Ninajaribu kusaidia lakini sio rahisi. Unatuma pesa zinareversiwa. Hata birthday nimetuma zawadi ikarudishwa. Hivyo inakuwa ngumu sana,” Mulamwah alimjibu shabiki aliyetaka kujua ikiwa anasaidia katika malezi ya bintiye.
Mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alibainisha kuwa haelewi tatizo liko wapi kati yake na mpenziwe huyo wa zamani.
Baadaye, Sonnie alionekana kuthibitisha kuwa huwa anamrudishia pesa na usaidizi mwingine alituma mpenzi wake wa zamani Kendrick Mulamwah kwa ajili ya malezi ya binti yao.
Mtayarishaji maudhui huyo alitoa taarifa fupi siku chache baada ya Mulamwah kuzungumza akiashiria sababu ya kutokubali usaidizi wa mpenziwe huyo wa zamani. Sonnie alizungumza kuhusu kutokubali ofa zinazokuja bila heshima.
"Habari za asubuhi. Kikumbusho tu cha haraka. "Haijalishi umefirisika kiasi gani, USIKUBALI kupokea matoleo yanayokuja na UKOSEFU WA HESHIMA," Sonnie aliandika.