Makumi ya mashabiki wa Magix Enga wameelezea wasiwasi wao baada ya mtayarishaji na mwimbaji huyo maarufu wa Kenya kutoa taarifa ya kutisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii huyo mwenye kipaji alichapisha picha ya kutisha ya uso wake uliokuwa umevimba uliokuwa umejaa michubuko na majeraha.
Katika sehemu ya maelezo, alifichua kuwa kuna mtu ambaye hakumtaja aliyejaribu kumtoa uhai alipokuwa mtaani.
“Karibu niuliwe na hater hapa kwa streets lakini Mungu ako na mimi, kesho ni siku nyingine tunatoa shukrani,” Magix Enga aliandika.
Mtayarishaji huyo ambaye amewahi kufanya kazi na baadhi ya wasanii wakubwa wa Kenya hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu kile kilichojiri.
Hata hivyo, kwa kuangalia sura yake kwenye picha aliyochapisha, inaweza kubainika wazi kuwa alikuwa amepigwa kwani hata alikuwa amevimba.
Kufuatia sasisho hilo, makumi ya wanamitandao wakiwemo wasanii wenzake wamejitokeza kuelezea wasiwasi wao kuhusu hatima ya mtayarishaji huyo na pia kuwasihi Wakenya wengine kumsaidia.
Tazama maoni ya baadhi ya watumiaji wa Instagram;
Officialmasauti: Daah magixx
Steve_muriuki: Huyu mwanaume anahitaji usaidizi wa kitaalamu. Tutapoteza mmoja wa wazalishaji bora nchini Kenya. Hizi posts mtazikumbuka wakati haihitaji.
Isaac_kaberere: Wacha pombe.
Dennisatwoli: Utaamka tena, kuna mwanga mwishoni mwa handaki.
_chavez_xx: Karibu wampige
Wanati_street: Huyu morio anapitia walai
Dj_flickyfit254: Huyu jamaa ana tatizo.. kinda depressed banaa.
Takriban miezi miwili iliyopita, mtayarishaji huyo wa muziki mwenye kipaji kweli alijitokeza kwa mara ya kwanza na kulia kwa uchungu jinsi ambavyo amekuwa akitaabika kutokana na mitikasi yake yote kubuma.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, alipakia picha yake akiwa amempakata mwanawe na kulia kuwa amejitahidi sana kuficha machungu yake lakini amefika mwisho kwani kila kitu ambacho anajaribu kukifanya kwa sasa hakileti tija.
Alifunguka kwamba licha ya kufanya kazi nyingi zilizotamba na wasanii wengi, hajawahi faidika kifhedha kutoka kwa kazi hizo hata moja, akitaja baadhi ya ngoma alizozizalishia midundo na kufanya vizuri lakini hajawahi faidika.
“Magix Enga, mfalme mwenye talanta wa beat barani Afrika kote na duniani. Baadhi ya wasanii niliofanya nao collabo walinufaika na Mimi. Nyimbo nyingi nilizotayarisha I.e (dundaing ,watoto na pombe Otile brown ft Enga and mejja , mapenzi hisia) na nyingine nyingi ambazo sinufaiki nao,” alisema.
Msanii huyo alisema licha ya mambo kumuendea mrama, bado anaamini kuwa yeye bado ndiye mzalishaji bora wa beat na kuendelea kuthibitisha hilo kwa kutaja baadhi ya kazi zenye midundo ya kuvutia alizowahi kuzalisha.
“Bado naamini mimi ndiye mtayarishaji bora. Mfano wimbo wa Gengetone watu waliupenda yaani wimbo unaokanyaga zaidi ni Mamiondoko ambao sijafaidika nao, Digidigi kutoka kwa Arrow boy ambao una views zaidi ya 10,000,000 sijapata hata senti moja kutoka kwake. Kwa sasa sina kazi,” alilia.
Alimalizia kusema kwamba yeye ni baba mpya mwenye mtoto mdogo ambaye anamtegemea lakini hana namna ya kumpa malezi bora.
Kutokana na masaibu yake, alimuomba rais Ruto kumpa msaada kuanzia kifedha hadi kwenye mkwamuo wa kisanaa.
“Sasa hivi naandika haya nina mtoto wa kiume wa mwezi 1 ambaye ananitegemea. Nilijaribu kujivuta lakini studio niliyokuwa nafanyia kazi ilifungwa kwa sababu ya masuala ya kukodisha. Rais wetu DR.William Samoei Ruto naweza kukuomba unisaidie katika usaidizi wowote unaoweza kuanzia tasnia ya muziki,” alimaliza.