Beka Flavour, mmoja wa wasanii wa bendi ya Bongo Fleva iliyosambaratika, Yamoto Band, ameomba mashabiki wake kwa moyo mkunjufu kumsaidia katika michango kwa ajili ya mahari ya mkewe.
Flavor katika mfululizo wa machapisho ya hivi majuzi aliwavunja moyo wengi kwa kudai kwamba mwaka 2023 haukuwa mzuri kwake kwani ndio mwaka ambao mke wake alimtoroka kwa kukosa kumlipia mahari.
Fleva alisema kwamba baada ya mkewe kuondoka, wazazi wake walimwekea vikwazo vingi ikiwemo kutoa mahari ya shilingi milioni 22 pesa za kitanzania kama wanataka arudi kwake na mtoto.
Beka amesema kwamba uwezo wa kutoa kiasi hicho cha pesa hana na kuomba msaada kutoka kwa wahisani wema kumwamua kabla ya wenye uwezo kumkwapua mkewe.
"Jamani kwanza samahani kwa wale wote ambao nimewakwaza kwa kumuomba msamaha mama watoto wangu, wapo walionipongeza lakini pia wapo walioniona mimi ni chizi/ punguani n.k…”
“… lakini bado kuna kikwazo hasa kwa familia yake mahari ambayo wanaitaka kutoka kwangu niwe mkweli siwezi kutoboa lakini nampenda binti yao sana, naombeni mchango please," msanii huyo alisema.
"Milioni 22 peke yangu siwezi nisaidie kabla wenye uwezo huo hawajapindua meza alafu nikaishia kula sembe na mkaishia kunisema vibaya zaidi ya mnavyonisema sasa hivi kuwa mimi ni mmoja wa wanaume wajinga,” aliongeza.
Beka alisema kwamba anahofia endapo atakosa kutoa kiasi hicho cha mahari hatoweza kumuona tena mkewe na mwanawe na kusema kuwa huenda akaathirika na msongo wa mawazo, hivyo kuwataka walimwengu kabla ya kuanza kumsema vibaya, wamsaidie kwanza.
“Ila naomba mtambue kitu kimoja kwamba msongo wa mawazo ya kimapenzi ni m'baya kuliko msongo wa kitu chochote hapa duniani"- aliandika Beka kisha kuweka namba yake ya mchango.
Beka ni mmoja kati ya wanachama wa Yamoto Band ambayo ilisambaratika kabla ya kila mmoja kuanza kufanya miziki binafsi.
Wenzake ni pamoja na Mbosso, Aslay na Enock Bella.