Muigizaji maarufu wa Kenya Caroline Muthoni almaarufu Carol Sonnie amefichua kwamba alipambana na msongo wa mawazo hadi kufikia hatua ya kukata nywele zake.
Mama huyo wa binti mmoja mnamo siku ya Alhamisi alichapisha video ya kumbukumbu iliyomuonyesha akiwa amekaa kwenye kinyozi akikatwa rasta zake.
Katika maelezo yake, alifichua kuwa alichukua hatua ya kukata nywele hizo ambazo alikuwa nazo kwa muda mrefu kama sehemu ya mabadiliko.
“Aki msongo wa mawazo karibu inichukue. Siku hii nilinyoa utambulisho wangu kwa mabadiliko. Let me tell you Maina. Sio rahisi," Carol Sonnie alisema chini ya video hiyo ambayo alishiriki kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Alisema kwamba angesema zaidi juu yake kwenye chaneli yake ya YouTube.
Kwa muda mrefu, mpenzi huyo wa zamani wa mchekeshaji Kendrick Mulamwah alijulikana kuwa na rasta nyeusi na kahawia kichwani.
Mama huyo wa binti mmoja aliwashangaza wengi aliponyoa rasta zake mnamo Septemba 2022 baada ya kuzifunga kichwani kwa takriban miaka tisa.
Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu katika siku za nyuma, muigizaji huyo alifichua kuwa aliweka rasta hizo mwaka wa 2013.
"Fikiria miaka tisa, niliiweka 2013 Septemba," Sonnie alijibu.
Pia alifichua kuwa alikuwa tayari kuuza nywele hizo baada ya kuzinyoa, lakini mnunuzi angelazimika kulipa 300,000 kwa ajili yake.