Sonko avunja kimya baada ya kushtumiwa kwa kumtumia vibaya Conjestina, afichua nani wa kulaumiwa

Sonko alishtumu familia ya bondia huyo wa zamani kwa kukatiza juhudi zake.

Muhtasari

•Wakenya walimshtumu Sonko kwa kumtumia Conjee kwa malengo ya kujipigia debe, huku akijifanya kumsaidia

•Sonko hata hivyo alidokeza kuwa atafanya jaribio la mwisho la kumsaidia bingwa huyo wa zamani wa ndondi.

katika hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network Hospital huko Miritini siku ya Jumamosi, Septemba 3, 2022.
Bingwa wa ndondi Conjestina Achieng na gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko katika hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network Hospital huko Miritini siku ya Jumamosi, Septemba 3, 2022.
Image: ONYANGO OCHIENG'

Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi, Gideon Mbuvi almaarufu Mike Sonko hatimaye amejibu kufuatia shutuma nyingi alizokabiliana nazo hivi majuzi kwenye mitandao ya kijamii baada ya hali ya sasa ya bondia wa zamani, Conjestina Achieng’ almaarufu Conjee kufichuliwa.

Mapema wiki hii, mwanahabari Carol Radul alitoa taarifa kuhusu hali ya bingwa huyo wa zamani wa ndondi wa Kenya akifichua kuwa amerudia mtindo wake wa zamani usio mzuri. Alibainisha kuwa juhudi zote ambazo yeye na wengine wameweka wakitumai kumsaidia hazijazaa matunda na hata akatangaza kuwa amekata tamaa.

Kufuatia ufichuzi huo, kundi la Wakenya lilimnyooshea vidole mwanasiasa Mike Sonko wakimshtumu kwa kumtumia bondia huyo wa zamani kwa malengo ya kujipendekeza kwa umma na kujipigia debe, huku akijifanya kumsaidia.

Katika majibu yake, mfanyibiashara huyo alitoa ushahidi wa juhudi nyingi alizoweka katika kumsaidia Conjee na akashutumu familia yake kwa kukatiza juhudi zake.

“Wakenya, nilijitahidi kumsaidia Conjee, lakini familia yake ilipunguza juhudi zangu. Kwa bahati nzuri, moyo wangu ni mkubwa kuliko mimi mwenyewe,” Sonko alisema kwenye taarifa.

Licha ya kusema juhudi zake zilikatizwa, Sonko hata hivyo alidokeza kuwa atafanya jaribio la mwisho la kumsaidia bingwa huyo wa zamani wa ndondi.

“Wakati fulani nashindwa kujizuia kwa upendo nilionao kwa watu hasa wasio na uwezo, na nadhani ndiyo sababu nilimpa Conjee la nafasi ya kwanza, ya pili, na sasa huenda nitalazimika kutoa nafasi ya tatu na ya mwisho tena kwa sababu siku zote huwa niko serious na kesi zote tunazochukua na kwa vile huwa tunaandika na kutoa hesabu kwa maendeleo ya kesi zetu zote nyeti,” alisema.

Sonko aliambatanisha taarifa yake na sauti ambazo alidai ni rekodi za mazungumzo ya simu aliyokuwa nayo na familia ya Conjee alipokuwa akijaribu kufuatilia hali ya bondia huyo wa zamani.

Katika chapisho lake la hivi majuzi, Bi Radull alibainisha kuwa hali ya bondia huyo wa zamani sio nzuri kwani mara kadhaa anakabiliana na nyakati mbaya.

Mwanahabari huyo aliwataka Wakenya wenye nia njema kuwa wanapitia nyumbani kwa bingwa huyo wa zamani katika eneo la Yala , wamsalimie na wamfanyie ununuzi kwani anapenda sana jambo hilo