Msanii wa kizazi kipya kutoka Tanzania, Alikiba amekuwa mtu wa hivi punde kutia neno lake kuhusu mchezo wa AFCON baina ya Taifa Stars ya Tanzania na timu ya taifa ya Morocco.
Alikiba kupitia instastory yake alionekana kuwalaumu wachezaji kwa kutokuwa katika viwango vyao bora lakini pia kuzembea uwanjani pasi na kujua kwamba walikuwa wanaliwakilisha taifa.
Alikiba alisema kwamba baadhi ya wachezaji katika kikosi cha Taifa Stars kilichochezea kichapo cha mabao 3-0 mikononi mwa Morocco walikuwa wanajichezea wenyewe badala ya kuwa wazalendo na kuipambania nchi.
“Kuchezea timu ya taifa ni tofauti kabisa na kucheza kwa ajili yako. Taifa Stars unatakiwa kucheza kwa ajili ya Tanzania, ila ndio matokeo ya mpira ila mechi ijayo tupambane kwa ajili ya Tanzania,” Alikiba aliwaasa wachezaji.
Taifa Stars waliduwazwa mikononi mwa Morocco huku wakionekana wabovu katika kila idarauwanjani kiasi kwamba hawakuweza kumalizia pasi zao na katika dakika zote 90, waliweza kupiga shoti moja tu na ambalo halikulenga langoni bali lilikwenda mbagombago.
Alikiba hata hivyo, aliwapongeza wachezaji hao kwa kujitahidi na kumaliza mechi hiyo na pia kuzuia kutofungwa mabao Zaidi, akisema kwamba timu ya taifa ya Morocco sio ya kawaida barani Afrika.
“Poleni kwa kazi kubwa mlioifanya kwa sababu Morocco sio timu ya kawaida Afrika,” alisema.
Itakumbukwa timu ya taifa ya Morocco imeimarika pakubwa katika siku za hivi karibuni haswa baada ya kuwashangaza wengi katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
Morocco ilikuwa timu ya taifa ya kwanza kutoka barani Afrika kutinga nusu fainali ya kombe la dunia, na hivyo kupigiwa upato kufanya vizuri hata Zaidi katika michuano ya Afcon Makala ya 2024 nchini Ivory Coast.
Licha ya kufanya vizuri katika kombe la dunia, Morocco imekuwa ikifanya vibaya katika michuano ya Afcon, ikiwa ni Zaidi ya miaka 47 tangu mara ya mwisho waliposhinda taji hilo.