Katika siku za hivi karibuni nchini Kenya, mjadala mkubwa umekuwa ukienezwa kuhusu mahusiano ya mapenzi ya wasichana ambayo aghalabu huenda mrama pindi baada ya kukutana na wanaume wanaowaalika kwenye mitoko.
Chini ya wiki mbili, wasichana 3 wamepatikana wameuawa kwa njia za utata, wawili kati yao wakipatana na umati wao katika nyumba za AirBnB ambapo wanakwenda kukutana na wanaume wao.
Mwanasoshoaliti Zari Hassan ambaye yuko nchini Kenya Kuitangaza chapa ya simu ya Samsung aliweza kuzungumzia mauaji haya ambayo wengi wameyataka kuwa yanawalenga watoto wa kike kidhalimu.
Akizungumza na Kalondu Musyimi wa Mpasho, Zari aliwashauri kina dada kuwa macho na watu ambao wanatoka nao kimapenzi haswa katika nyumba za Airbnb.
Zari alisema kwamba ni wakati sasa wasichana kujijali Zaidi na kuweka maisha yako kipaumbele badala ya kuweka maslahi yao mbele na kuendekeza mapenzi bila kujua kuwa ni mtego wa mauti.
“Nafikiri tunahitaji kuwa macho Zaidi, mauaji yale yalikuwa ya kinyama sana niliona kwenye TikTok, niliona miili ikiwa inapakiwa kutoka kwa nyumba, AirBnB, kwa kweli kina dada, kama kweli unahitaji kwenda kwenye hizo dates, hakikisha unawataarifu watu wako wa karibu unaenda wapi na unaenda kukutana na nani na vitu kama hivyo,” Zari alishauri.
Haya yanajiri wakati ambapo familia ya mrembo aliyeuawa Roysambu kwenye AirBnB ikijitokeza na kudai kwamba mtoto wao aliuawa na mtu aliyemteka nyara baada ya kumbembeleza hadi kukutana kwenye nyumba hiyo.
Familia ya msichana huyo, Rita Waeni ilisema kwamba walipokea jumbe kutoka kwa muuaji huyo alitaka kima cha nusu milioni ili kumuachia mpendwa wao lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kupata kiasi hicho.
Mwili wa Rita Waeni ulipatikana umewekwa kwenye mfuko wa gunia na kutupwa nje ya nyumba hiyo kando ya barabara, huku ukiwa vipande vipande.
Kufikia sasa, kichwa chake bado hakijapatikana.