Jamaa mchekeshaji kwa jina Clam Vevo anayejidai kuwa ni mpenzi wa zamani wa msanii Zuchu amefunguka kwa undani jinsi mapenzi yao yaligonga mwamba baada ya mrembo huyo kusainiwa chini ya lebo ya WCB.
Jamaa huyo katika mahojiano ya kihisia na blogu moja alielezea kwamba walianza mapenzi yao mwaka 2015 kipindi hicho wote wakiwa na maisha ya chini lakini baada ya Zuchu kuanza kushika hela, kulitokea na mwanya mkubwa katika maisha yao kupelekea penzi kufa.
“Kiukweli yeye ndiye mtu ambaye alinifanya mpaka leo hii watu wanaona Clam anafanya vizuri, hawajui chanzo chake, lakini chanzo ni Zuchu. Kwa hiyo ni maneno yake, namna ambavyo maisha tuliyoishi, mahusiano yetu namna yalivyokufa, ilinitia hasira sana kupambana Zaidi,” alisema.
Clam alizungumzia ujumbe aliochapisha kwenye Instagram wiki jana baada ya Diamond kusema kwamba ameachana na Zuchu.
Mchekeshaji huyo alichapisha ujumbe wa kumuomba Zuchu kumrudia akisema kwamba kwa sasa ameshakuwa mtu mwingine tofauti na alivyomuacha.
Alisema kwamba haikuwa kiki bali alikuwa anazielezea hisia zake, akiwa na Imani kwamba Diamond alikuwa amemaanisha maneno yake kuwa yuko single na hayuko na Zuchu tena.
“Nilikuwa nazielezea hisia zangu pale, nikazungumzia kila kitu na kumkaribisha kwenye maisha yangu rasmi kwa mara nyingine. Nilimwambia maisha yamebadilika, venye nilivyokuwa sivyo nilivyo sasa hivi,” alieleza.
Hata hivyo, alitamaushwa baada ya kuona tena Diamond ametengua kauli yake ya awali kuwa ameachana na Zuchu, lakini alisema kwamab kuelezea hisia zake alikuwa anaamini kwamba walikuwa wameachana.
“Maisha yana vitu vingi sana, watu wanapitia mambo mengi sana kwenye maisha, niliona watu wakisema eti mimi na Zuchu ni wapi na wapi. Lakini wao hawajui kwamba mimi simzungumzii Zuchu wa sasa, namzungumzia Zuhura wa 2015. Watu wenye wanaelewa na wanakumbuka wanatambua jinsi mimi na Zuhuru tulikuwa tunapendana.”
“Mimi natambua ni kiasi gani yeye ananipenda, sababu kubwa yeye kuniacha ilikuwa ni pesa. Issue kubwa yeye kuanza kuzinguana na mimi ni alipochukuliwa na kusainiwa WCB. Baada ya kusainiwa, kuna namna ikawa kama tumechana na pengo kubwa na ikatokea hivyo kwa sababu kipindi hicho ndio nimetoka kijijini nimekuja mjini na sijajitambua sana,” aliongeza.