Nay wa Mitego avunja kimya kufuatia madai alikejeli Kenya katika wimbo wake mpya

Rapa huyo alibainisha kuwa hakutaja nchi yoyote katika wimbo huo ambao alitoa siku chache zilizopita.

Muhtasari

•Nay wa Mitego amekanusha madai kwamba aliimba kuhusu Kenya katika wimbo wake mpya zaidi wa ‘Wapi Huko.’

•Nay alibainisha kuwa wengi wa watu ambao walijibu wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii ni Wakenya

wa Nay wa Mitego ulizua mjadala Kenya
Wimbo wa Nay wa Mitego ulizua mjadala Kenya
Image: INSTAGRAM// NAY WA MITEGO

Rapa maarufu wa Tanzania Emmanuel Elibarick almaarufu Nay wa Mitego amekanusha madai kwamba aliimba kuhusu Kenya katika wimbo wake mpya zaidi wa ‘Wapi Huko.’

Wimbo tata wa kejeli wa kisiasa wa Nay wa Mitego umevuma nchini Kenya katika siku chache zilizopita huku Wakenya wengi wakihisi kuwa unaangazia matatizo yaliyomo nchini.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, rapper huyo wa bongo fleva hata hivyo aliweka wazi kuwa hakutaja nchi yoyote katika wimbo huo alioutoa siku chache zilizopita.

“Wimbo wangu mpya #WapiHuko sijataja jina la nchi lakini jirani zetu Kenya naona wameamua kuuchuka huu wimbo na kusema ni wao. Yaani nimewaimbia wao kufatana hali ya maisha ya nchi yao kwa asilimia 90/100%,” Nay wa Mitego alisema kupitia Instagram.

Nay alibainisha kuwa wengi wa watu ambao walijibu wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii ni Wakenya ambao walidhani kuwa unawahusu.

“Naona comments nyingi sana za Wakenya tangu hana mpaka hivi sasa. Pale Youtube na kwenye page za media na wadau kadhaa nchini Kenya!,” alisema.

Aliongeza, “Lakini pia Watz nao hawapo nyuma kujibu kufatana na hali yao pia wanasema Wakenya tulieni wimbo unahusu Tanzania asilimia 90/100%. Kupitia wimbo huu #WapiHuko, tunapata majibu nchi zetu hizi mbili. Jirani Kenya na Tanzania juu ya maisha yao na viongozi,”

Rapa huyo aliendelea kuwataka mashabiki wake watoe maoni yao kuhusu nchi ambayo wanadhani aliimba kuhusu.

Wakenya waliachwa vinywa wazi kufuatia wimbo huo wa Nay wa Mitego, uliozungumzia kuhusu nchi isiyojulikana.

Wimbo huo wa “Wapi huko” unaangazia taifa` fulani linaloandamwa na uongozi mbovu, rushwa, njaa na ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wake.

Katika wimbo huo, Nay anasimulia jinsi nchi inavyoonekana kuwa nzuri na yenye mafanikio mbele ya ulimwengu, lakini watu wake wanateseka chini ya viongozi wazembe, vijana wake wanasota kwenye umasikini na wasichana wake sasa wameingia kwenye pesa kuliko mapenzi.

Zaidi ya hayo, rapa huyo anawachana vijana kwa kuwatafuta akina kina mama wenye fedha, kuzungumza Kiingereza kizuri na kujigamba jinsi nchi yao ilivyo bora kuliko majirani zao, lakini nyumbani kwao hawana hata umeme.