Esther Musila awajibu wanaokejeli umri wake akiomboleza rafikiye aliyeaga siku 7 kabla ya birthday

Mkewe Guardian Angel alisherehekea umri mkubwa akisema maisha ni baraka kutoka kwa Mungu.

Muhtasari

•Musila alizungumza jinsi marehemu alitarajia kufikia umri wa miaka 50 lakini kwa bahati mbaya akaaga siku chache kabla ya kufika hapo.

•Pia alikashifu wale wanaokejeli wengine kuhusu umri wao akisema ataendelea kuzeeka bila kujuta

Esther Musila
Image: INSTAGRAM

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za Injili Guardian Angel, Bi Esther Ngenyi Musila alihudhuria ibada ya mazishi ya marehemu rafiki yake mnamo Jumatano asubuhi.

Mama huyo wa watoto watatu alifichua hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alieleza kwamba marehemu aliaga wiki moja tu kabla ya siku yake ya kuzaliwa ya 50.

Musila alizungumza jinsi marehemu alitarajia sana kufikia umri wa miaka 50 lakini kwa bahati mbaya akaaga siku chache kabla ya kufika hapo.

“Leo asubuhi nilihudhuria ibada ya mazishi ya rafiki yangu. Leo ingekuwa siku yake ya kuzaliwa ya 50,” Esther Musila aliandika Jumatano.

Aliongeza, "Alikuwa akitarajia hatua hii kubwa maishani mwake, haikufanyika, aliaga siku saba kabla ya siku yake ya kuzaliwa."

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alitumia fursa hiyo kusherehekea umri mkubwa akisema maisha ni baraka kutoka kwa Mungu. Pia alikashifu wale wanaokejeli wengine kuhusu umri wao akisema ataendelea kuzeeka bila kujuta.

“Watu wanapokutukana kwa sababu ya umri wako, huwa wanafikiri ni Mungu ndiye anayepeana uhai na si wao? Nitaendelea kuzeeka kwa uzuri na bila msamaha!!,” alisema.

Bi Musila alichapisha picha na video zinazoonyesha jinsi walivyosherehekea marehemu rafiki yao na jinsi walivyoadhimisha ambayo ingekuwa siku yake ya kuzaliwa.

Pia alipata kukutana na kinara wao katika shule ya upili na marafiki wengine wa zamani wakati wa ibada ya mazishi ya rafiki yao.

Kwa muda mrefu, mama huyo wa watoto watatu amekuwa akikejeliwa kutokana na tofauti kubwa ya umri kati yake na mumewe Guardian Angel. 

Musila ambaye amempiku umri Guardian Angel kwa takriban miongo miwili alifunga pingu za maisha na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili mwanzoni mwa mwaka wa 2022 na wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha. Hata hivyo, si kila mtu anafurahia ndoa yao kwani baadhi ya Wakenya wamekuwa wakikosoa muungano wao na kumkosoa kwa kuolewa na mwanamume ambaye ni mdogo zaidi yake.