Shule ya zamani ya muigizaji Charles Ouda yafichua maelezo kumhusu huku ikimuomboleza

St Mary's ilifichua kuwa muigizaji huyo marehemu alikuwa nahodha wa bweni wakati alipokuwa mwanafunzi.

Muhtasari

•Shule hiyo ya kifahari ilimuomboleza marehemu Ouda kama mwanamume ambaye alipenda sana uigizaji na usanii.

•Shule hiyo ilifichua kwamba hata baada ya kumaliza masomo yake, bado angerudi huko ili kuwatia moyo wanafunzi wengine.

CHARLES OUDA
CHARLES OUDA
Image: HISANI

Shule ya St Mary’s- Nairobi imeomboleza mwigizaji wa Kenya marehemu Charles Ouda almaarufu ‘Charli’.

Katika barua ya rambirambi iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na mchumba wa Ouda Ciru Muriuki, shule hiyo ya kifahari ilimuomboleza marehemu Ouda kama mwanamume ambaye alipenda sana uigizaji na usanii.

Shule hiyo ilisherehekea miaka kumi na tatu ambayo muigizaji huyo alikuwa mwanafunzi pale na kufichua kwamba hata baada ya kumaliza masomo yake zaidi ya miongo miwili iliyopita, bado angerudi huko ili kuwatia moyo wanafunzi wengine wakati wa hafla za sanaa shuleni.

Tunahuzunishwa kujua kuhusu kifo kisichotarajiwa cha mwanafunzi wetu wa zamani Charles J Ouda. Tunamkumbuka Charles akiwa mvulana mdogo alipojiunga nasi mwaka wa 1990 katika darasa la 1, hadi 2003 alipomaliza programu ya IB,” ilisomeka sehemu ya barua ya Shule ya St Mary’s," Barua hiyo ilisomeka.

Barua hiyo ilisomeka zaidi, "Charles alikuwa mtu mcheshi ambaye alikuwa akipenda sana uigizaji na usanii na pia alikuwa akija kuhamasisha wasanii mbalimbali wakati wa muziki wa shule kwa miaka mingi. Roho yake ipumzike kwa amani ya milele. Kwa huruma nyingi.”

Katika barua hiyo, shule hiyo ilizidi kufichua kuwa muigizaji huyo marehemu alikuwa nahodha wa bweni wakati alipokuwa mwanafunzi.

Aidha, walishiriki nukuu ya zamani ya motisha ya muigizaji hiyo iliyosoma, "Katika maisha, tuna chaguo mbili. Tunaweza kuongoza au kufuata. Kwa miaka yangu yote katika St. Mary's, niliheshimiwa kufuata njia iliyopangwa vizuri kwa ajili yangu.

Katika kila muziki, michezo, na shughuli iliyochukuliwa, nilipata mengi kutoka kwa wale walioongoza. Sasa, simu za maisha na uzoefu wa hapa, nimejifunza kwamba sihitaji tena kufuata, hatima yangu ni kuongoza."

Ouda alikuwa mwigizaji, mwandishi, mkurugenzi, mtangazaji wa TV, msanii wa sauti na mwimbaji ambaye alianza kazi yake mnamo 2002.

Mara ya mwisho alionekana akiwa hai akihudhuria hafla iliyoandaliwa kwa waigizaji wa kipindi cha Maisha Magic ‘Salem Show.’

Alipokuwa akitangamana na marafiki zake wakati wa hafla hiyo, mwigizaji huyo aliwahimiza kukamata kila wakati maishani akisema "walinusurika".