"Ni bora kuondoka mapema" Akothee awaonya wanawake dhidi ya kupigania ndoa zinazokufa

Mwanamuziki huyo amewashauri wanawake walioolewa kuwa tayari kugura ndoa zao pindi zikianza kuyumba.

Muhtasari

•Akothee alibainisha kuwa kuna wanawake wengi ambao wamepoteza maisha wakijaribu kupigania ndoa ambazo zimeshindwa kufanya kazi.

•Alibainisha kuwa kuna wanawake wengi sana ambao wamewapoteza waume zao, sio kwa kifo, bali wamewapoteza kwa dunia.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth Kokeyo almaarufu Akothee amewashauri wanawake dhidi ya kusalia katika ndoa zisizofanya kazi.

Katika taarifa yake ya Ijumaa jioni, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwashauri wanawake walioolewa kuwa tayari kugura ndoa zao pindi zikianza kuyumba.

Alibainisha kuwa kuna wanawake wengi ambao wamepoteza maisha wakati wakijaribu kupigania ndoa zao ambazo zimeshindwa kufanya kazi.

“Uchungu wa mwanamke kupoteza mume kwa mwanamke mwingine au kwa ulimwengu unahitaji uchunguzi wa kina. Hatima inaonekana, lakini itachukua miaka, haswa wakati huwezi kujidhibiti kama mwanamke. Chaiii, mwanaume kabeba kitanda chako na yeye. Kadiri unavyoondoka mapema, ndivyo bora kwako,” Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Mama huyo wa watoto watano alibainisha kuwa ni bora mwanamke arudi nyumbani kwa wazazi wake akiwa hai kuliko kupoteza maisha wakati akiwa anapigania ndoa yenye matatizo na kurudishwa nyumbani kwenye jeneza.

“Nimeona wanawake wakipoteza maisha kwa jina la kupigania ndoa zao zifanye kazi. Afadhali aje nyumbani ndani ya Matatu na sio juu ya Matatu. Rudi nyumbani na jina Esther Akoth Kokeyo badala ya "Mwili unawasili kesho" Akothee aliandika.

Mwanamuziki huyo alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akimtambua rafiki yake mmoja ambaye anaendesha mpango unashughulika na kusaidia wajane.

Alibainisha kuwa kuna wanawake wengi sana ambao wamewapoteza waume zao, sio kwa kifo, bali wamewapoteza kwa dunia.

"Wanawake wengi wana waume waliokufa katika mwili unaosonga, unaozunguka ulimwenguni kote, na kusababisha maumivu yasiyo ya lazima. Maumivu ya kufiwa na mume ni ya kuumiza sana, lakini angalau unapata hitimisho unapopita na kumuona pale kando ya nyumba,” alisema.

Haya yanajiri miezi michache baada ya mama huyo wa watoto watano kuigura ndoa yake iliyodumu kwa muda mfupi na Denis Schweizer, ambaye alikuwa amempa jina la utani ‘Omosh’.

Akothee alitoroka ndoa yake na Omosh mnamo Juni mwaka jana, miezi miwili tu baada ya kufunga pingu za maisha na mzungu huyo kutoka Uswizi.