"Si uchawi, ni sayansi!" Gidi azungumza baada ya utabiri wake wa Kombe la Dunia na Afcon kutimia

Mtangazaji huyo mahiri amesema kwamba utabiri wake sahihi si kwa sababu ya uchawi bali ni Sayansi.

Muhtasari

•Huko nyuma mnamo mwaka wa 2022, mwimbaji huyo wa zamani alitabiri kwamba Argentina ingeshinda kombe la dunia. 

• Mwaka huu, pia alitabiri kwamba mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, Ivory Coast angeshinda kombe hilo.

Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji mahiri wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi amesherehekea baada ya utabiri wake kuhusu Kombe la Dunia 2022 na Afcon 2023 kutimia.

Huko nyuma mnamo mwaka wa 2022, mwimbaji huyo wa zamani alitabiri kwamba Argentina ingeshinda kombe la dunia. Mwaka huu, pia alitabiri kwamba mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, Ivory Coast angeshinda kombe hilo.

Kwa kweli, kama alivyotabiri, timu ya Argentina ilishinda Kombe la Dunia lililochezwa nchini Qatar mnamo Novemba na Desemba 2022 huku Ivory Coast ikiwapiga Super Eagles wa Nigeria mnamo Jumapili, Februari 11, 2023 na kushinda Afcon 2023.

"Nilitabiri ARGENTINA kutwaa Kombe la Dunia 2022 na ikawa hivyo, nilitabiri IVORY COAST kutwaa AFCON 2023 na ikawa hivyo," Gidi alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu asubuhi kufuatia kumalizika kwa Afcon 2023 Jumapili usiku.

Mtangazaji huyo mahiri aliendelea kusema kwamba utabiri wake sahihi si kwa sababu ya uchawi bali ni kwa sababu ya Sayansi.

"Sio uchawi, ni sayansi tu," alisema.

Baada ya fainali ya Kombe la Dunia la 2022 kuchezwa na Argentina kutwaa ushindi, Gidi alisherehekea kuwa utabiri wake wa mshindi wa mashindano hayo ulitimia.

"Kuanzia Siku ya kwanza, na kuendelea, niliwaambia Argentina inashinda Kombe la Dunia, iwe kwa bahati, penalti na gik ma kamago, ushindi ni ushindi na Messi ndiye mshindi wa Kombe la Dunia la 2022. Chukua hustler fund unitumie,” Gidi aliandika kwenye mtandao wa Facebook.

Katika chapisho lingine la Facebook mnamo Januari 13, msanii huyo wa zamani wa kundi la muziki la Gidi Gidi Maji Maji alisema kuwa hata kama alikuwa akiishabikia timu ya Cameroon, alihisi kuwa Ivory Coast ingeshinda kombe la Afcon.

“Nilitabiri kwa usahihi washindi wa mwisho wa Kombe la Dunia Argentina kabla ya kuanza. Kufikia Afcon mwaka huu, nadhani itaenda kwa Ivory Coast ingawa ninakimbilia Cameroon," alisema.

Mnamo Januari 13, alishikilia utabiri wake akisema, "Utabiri wangu niliotoa kabla ya mashindano kuanza bado upo, Cote d'Ivoire inashinda AFCON 2023."

Pia alisisitiza msimamo wake mnamo Februari 4.