Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza amesherehekewa kimapenzi na mumewe Robert Murega Baichu leo ikiwa Siku ya Wapendanao.
Mwimbaji huyo alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kumsherehekea bosi huyo wa kaunti ya Meru na kumhakikishia kuhusu mapenzi yake mazito kwake.
Katika taarifa yake kwa mkewe. Murega Baichu alibainisha kuwa huwa hachoki naye na kusema kwamba anataka kumpa zaidi.
“Sitosheki kwako. Ninataka tu kukupa zaidi,” Murega Baichu aliandika kwenye Facebook.
Aliambatanisha kauli yake na picha nzuri yake na gavana huyo wa Meru wakionekana kuwa na furaha pamoja na kuzama kwenye mahaba mazito.
"Kheri ya Siku ya Wapendanao Hon Kawira Mwangaza," Murega Baichu aliandika.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, Gavana Kawira Mwangaza alimmiminia sifa hadharani mume wake Robert Murega Baichu, wiki chache tu baada ya kunusurika kuondolewa madarakani.
Alipokuwa akitoa mahubiri katika ibada katika Kanisa la Jesus House of Praise, mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alimtawaza mumewe kwa vyeo vikubwa vikubwa katika harakati za kumsherehekea.
"Anaitwa mume wa gavana mwenyewe, ndiyo, mume wa gavana mwenyewe," Kawira Mwangaza aliwaambia washarika waliokuwa wamehudhuria ibada hiyo kwa ujasiri.
Aliendelea kujigamba kuhusu kuwa na mwanamume mwenye sura nzuri zaidi na akazungumza kuhusu jukumu kubwa la mwanamuziki huyo katika taaluma yake ya kisiasa.
“Yeye ndiye kamanda wa Shirika la Ndege la Ameru, mwenye sura nzuri zaidi barani Afrika na baadhi ya sehemu za Ulaya. Mshauri wa kisiasa wa gavana wa Kaunti ya Meru, na John Mbatizaji wa leo kwa gavana,” akasema.
Gavana Kawira Mwangaza pia hakumaliza mahubiri yake bila kujigamba kuwa mke kamili.
“Ndiye mwanamume pekee aliyebarikiwa kuwa mke anayestahili. Mwanaume pekee mwenye wife material. Makofi kwake jamani,” alisema.