Ombi maalum la Bahati na Diana Marua kwa binti yao wa mzaliwa wa kwanza

Bahati na Diana Marua wamemsherehekea mzaliwa wao wa kwanza, Heaven Bahati anapoadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Muhtasari

•Heaven aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya sita mnamo Jumatano, Februari 14 na wanandoa hao walimwandikia jumbe nzuri.

•Diana Marua alifanya maombi maalum kwa ajili ya bintiye ambapo alimwomba Mungu amuongoze na kumlinda.

Diana Marua na binti yao Heaven Bahati
Image: INSTAGRAM// HEAVEN BAHATI

Wanandoa mashuhuri Kelvin Bahati na Diana Marua wamemsherehekea mzaliwa wao wa kwanza Heaven Wendo Bahati anapoadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Heaven ambaye ni mtoto wa pili wa Bahati aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya sita mnamo Jumatano, Februari 14 na wanandoa hao walimwandikia jumbe nzuri.

Katika ujumbe wake, Diana Marua alimtaja binti yake kuwa baraka yake ya kwanza na tunda la kwanza la tumbo lake.

"Siku kama hii miaka 6 iliyopita, tulishikilia zawadi ya thamani zaidi ya maisha yetu. Limbuko la tumbo langu. Baraka yangu ya kwanza, Muonekano Wangu, Upendo Wetu, Mbingu Yetu Duniani, Mtoto Wetu  wa Valentine’s❤️. Najivunia kuitwa Mama yako,” Diana Marua aliandika kwenye Instagram.

Mama huyo wa watoto watatu alionyesha upendo wake mkubwa kwa binti yake ambaye alifichua kuwa anajiamini na kuwajibika.

Pia alifanya maombi maalum kwa ajili ya bintiye ambapo alimwomba Mungu amuongoze na kumlinda.

“Umetufanya tuwe na kujivunia sana. Tunampenda Malaika ambaye unakua  kuwa. Kujiamini na wajibu wako kama dada mkubwa ni wa kupendeza,” alisema.

Aliongeza, “Unapokua, tunaomba kwamba Mungu aongoze njia zako na kuulinda moyo wako. Utakuwa mtoto wetu kila wakati hata ikiwa unazidi mikono yetu. Tunakupenda sana na hatuwezi kusubiri kukuona ukikua kufanya maamuzi yako mwenyewe. Heri ya siku ya kuzaliwa Wendo wetu."

Kwa upande wake, Bahati alisherehekea tabia nzuri za bintiye na kumwomba Mungu ambariki.

“Kukupa jina la Wendo ilikuwa kama Unabii kwa sababu Binti Yangu umejaa Upendo; moyo wako ni safi na unaijaza nyumba yetu kwa Furaha nyingi. Mungu akubariki na akulinde. Maisha Marefu na Mafanikio ni sehemu yako kwa Jina la Yesu,” Bahati aliandika.

Heaven ni mtoto wa kwanza wa Bahati na Diana Marua wakiwa pamoja. Wanandoa hao ambao wamekuwa pamoja kwa takriban miaka saba wana watoto wengine wawili pamoja.