Muigizaji mashuhuri wa Kenya Caroline Muthoni Ngethe almaarufu Carol Sonnie amefunguka kuhusu mapambano yake na msongo wa mawazo katika kipindi cha nyuma.
Katika mahojiano na wanahabari wa mtandaoni, mama huyo wa binti mmoja alikiri kwamba aliathirika kisaikolojia baada ya mahusiano yake kufeli na ilimbidi kutafuta usaidizi kutoka kwa mtaalamu.
Alisema kuwa msongo wa mawazo ulimsumbua sana hivi kwamba hata muonekano wake wa mwili ulibadilika na kuzua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wake.
“Wakati huo kuna mtu aliniuliza, ama Sonie uko na UKIMWI. Aki nilikuwa nimebeat. Kusema kweli niliulizwa swali hilo hadi nikaenda kupimwa. Na najua tu vizuri sina,” Carol Sonnie alifunguka.
Aliongeza, “Kwa upande wangu, nilikuwa najiona niko sawa. Nikijiangalia kwa kioo nilikuwa naona niko sawa. Sikuwa najua hiyo kitu imeniathiri kiakili. Ilikuwa inanimaliza nguvu sana.”
Mpenzi huyo wa zamani wa mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah hata hivyo alimshukuru mwanasaikolojia wake akifichua kwamba alimsaidia kukabiliana na msongo wa mawazo.
"Nadhani kwa kweli nilienda kwa mtaalamu bora katika ulimwengu huu. Alinisaidia sana kujijua na kujielewa. Sidhani kuna kitu kinaweza kunirudisha nyuma hadi mahali ambapo nilikuwa kwa sababu kama huko sawa kiakili, nilikuwa nakula sana lakini siongezi uzani,” alisea,a
Sonie alibainisha kuwa amani ya akili ni muhimu sana kwa maendeleo ya kibinafsi.
Mama huyo wa binti mmoja pia alifichua kuwa wazazi wake wamemuunga mkono sana haswa katika malezi ya bintiye wa pekee, Keilah Oyando.
Takriban miaka miwili iliyopita, Carrol Sonie alilemewa na hisia studioni zetu alipokuwa akisimulia kuhusu athari za baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake, mchekeshaji Mulamwah.
Katika mahojiano na Massawe Jappani, Muthoni alikiri kuwa matukio yaliyofuata baada ya kutangaza kutengana kwake na Mulamwah yalimuathiri vibaya kiasi cha kwamba alishindwa kunyonyesha bintiye.
"Kusema kweli, sasa nimepona. Iliniathiri sana. Ilifika wakati hata singeweza kunyonyesha mtoto. Maziwa ilikuwa imeisha. Mamangu alikuwa anachukua simu yangu ili nisisome jumbe. Niliathiriwa na msongo wa mawazo. Ni mwanamke tu ataweza kuelewa hali hiyo. Nashukuru kuwa mtoto wangu anaendelea vizuri lakini hapo awali ilikuwa ngumu kwake," Muthoni alisema.
Muthoni alisema wazazi wake pamoja na baadhi ya marafiki na mashabiki walimsaidia sana kupambana na msongo wa mawazo ambao ulikuwa umemuathiri.
Wakati huo, muigizaji huyo aliweka wazi kuwa tayari ameweza kusonga mbele na maisha yake. Hata hivyo alikiri kuwa anampeza sana Mulamwah katika maisha ya binti yao.
"Kusema kweli nilitaka mahusiano yetu yafanye kazi. Lakini kwa kuwa mambo yalienda jinsi yalivyoenda lazima tusonge mbele na maisha na tuzoee. Napeza uwepo wake hasa kwa maisha ya mtoto wangu. Ningependa ahusike zaidi katika malezi," Muthoni alisema.