Wanasema binadamu hukutana, milima tu ndio haiwezi kukutana!
Miezi kadhaa baada ya kutupiana cheche za maneno kwenye mitandao ya kijamii, hatimaye bosi wa bodi ya hakimiliki za kazi za Sanaa nchini MCSK, Ezekiel Mutua amekutana na msanii Sylivia Ssaru, muimbaji wa wimbo maarufu miongoni mwa vijana – Kaskie Vibaya.
Wawili hao ambao walidhaniwa kuwa ni maadui wa kutopikika kwenye chungu kimoja walikutana katika hafla ya tuzo za Pulse, PMVA usiku wa Jumatano.
Tuzo hizo zinazotambua na kukuza muziki wa Kenya huandaliwa na jarida la Pulse lililoko chini ya shirika la habari la Standard, na hafla yenyewe ilifanyika katika mgahawa wa Nairobi Street Kitchen, mtaani Westlands, Nairobi.
Mutua kwa furaha alisema kwamba yeye sasa ni mshauri wa Ssaru ambapo aliweka wazi kwamba kilichotokea miezi kadhaa iliyopita haikuwa chuki dhidi yake bali alikuwa anajaribu kumnyoosha katika njia salama kisanaa.
Mutua alisema sasa wanaweza sema ni ‘Kaskie Vizuri’ akibananga maana ya wimbo uliozua bifu baina yao, ‘Kaskie Vizuri’ Ssaru akishirikishwa na Fathermoh.
“Mshauriwa wangu mpya Sylvia Saru sasa anasema "Kaskie Vizuri." Tunasherehekea wabunifu wetu wachanga wanaothamini nguvu ya muziki na juhudi tunazofanya ili kufanya muziki uheshimike na kuleta faida,” Mutua aliandika.
Mwezi Juni mwaka jana, Mutua alionyesha kukasirishwa na maudhui yaliyomo katika kolabo ya Fathermoh na Ssaru – Kaskie Vibaya – akisema kwamba wimbo huo unapotosha jamii.
Mutua alisema kuwa kwa kuendelea kutoa nyimbo zenye maudhui chafu, wasanii wanawafurahisha watu wasiowajua mitandaoni na kupewa tu ahasante ya mdomo huku wakiendelea kujitenga mbali na makampuni ya kibiashara ambayo yangewapa mkataba wa hela nono kama mabalozi wao, kwani makampuni mengi hayawezi kujihusisha na watu wenye maudhui chafu.
“Kwa hiyo unafanya wimbo mmoja mchafu na inakufika kichwani hadi ukatupilia mbali ushauri wa wazee na wataalamu waliobobea kwa kuwafukuza kwa kuwapungia mkono "Kaskie Vibaya na huko kwenu?" Mutua aliuliza.
“Halafu wageni wanapandisha matusi na majivuno yako kwenye mitandao ya kijamii na kujiona uko juu ya dunia. Ni wimbo uliovuma katika vilabu vyote vya usiku. Lakini vituo na vilabu vya usiku vinavyotumia wimbo wako havikulipi chochote, au kama kuna chochote, karanga. Kwa kweli mashirika mengi hayahusishi chapa zao na uchafu kwa hivyo unajitenga na pesa nyingi huku ukifurahisha watu wasiowajua kwenye mitandao ya kijamii,” Mutua aliongeza.