Mchungaji wa kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a amevunja kimya chake baada ya kuhudhuria mkutano mkubwa wa maombi katika uwanja wa Nyayo Jumamosi, mkutano ulioongozwa na mwinjilisti kutoka Marekani, Benny Hinn.
Akizungumza Jumapili kaitka ibada kanisani mwake, Ng’ang’a alisema kwamba mwinjilisti huyo wa Marekani mwenye asili ya Israeli alikuwa na wakati mgumu sana kuonyesha kipaji chake cha kuhubiria watu, japo akamsifia kwa kuimba vizuri.
“Nilikuwa kwenye ule mkutano, nilikaa hapo kwa sababu nilienda tu kuangalia vile Mungu anamtumia. Sitaongea sasa hivi, lakini kulikuweko na kitu si sahihi mahali Fulani. Yule mtu ali’struggle. Ali’struggle, ni mwimbaji, aliimba nyimbo nikiwa hapo aliimba sana mpaka apate pale… na mimi nilijua hapa ndipo hapa na hapa, mimi ni mtu wa hesabu,” Ng’ang’a alisema.
Hata hivyo, mchungaji huyo anayejiita Kamanda mkuu katika jeshi la Bwana alisema kwamba hakutambuliwa inavyostahili kwa heshima zote, kwani alitengwa kando na mbali kwenye kimeza kidogo.
“Mimi nilikuwa nimewekwa kule, kameza kalikuwa pale. Hata nilitajwa na mtu mmoja tu, ‘Kenya One yuko hapa’… lakini wale walikuwa pale mbele wote, angalia wote [jinsi walivyotambuliwa]…” Ng’ang’a alilalamika.
Pasta Ng’ang’a alidokeza kwamba alitoka kule na funzo kuu la kuzingatia mambo yake na kutoenda sehemu asiyoalikwa.
“Nilitamani tu nipewe gitaa tu nipige hata nyimbo mbili waone deliverance ile ingefanyika hapo, lakini unaona Kenya haiwezi kunipokea mimi. Wanapokea Waganda, wao ndio wanapewa kiti. Niliona Pasta Ezekiel alikuwa amekaa mahali karibu na mlango, alitoka mbele yangu… hata kuambiwa ufanye mkono hivi [hewani kusalimia watu] hakuna,” alisema.
“Mimi nilikuwa tu naangalia vile Mungu ananitumia na vile anamtumia pia yeye [Benny Hinn] nikajua hata mimi nipo. Hata serikali ya Kenya msiponitambua, serikali ya Mbinguni inanitambua,” aliongeza.