Harmonize amekanusha kumiliki lebo ya muziki iitwayo Konde Music Worldwide.
Msanii huyo wa ‘Single Again’ kupitia insta story yake alisema kwamba yeye anamiliki ‘Konde Gnag’ ambalo linakaa Zaidi kama kundi la kihuni kuliko kuonwa kama lebo ya muziki.
Alisema kwamba anachokimiliki ni ‘gang’ ya watu wawili tu – yeye na Ibraah.
Hata hivyo, alisisitiza kauli yake ya wiki jana kwamba hivi karibuni atawasaini wasanii wengine wawili wapya wenye kipaji cha kipekee.
Katika sasisho hilo, Harmonize aliwataka mashabiki wake kuendelea kumtegi kwenye wasanii chipukizi wenye talanta na ambao wanaona kama wakishikwa mkono na Konde Gang basi nyota yao itang’aa.
“Kusemi ukweli mimisimiliki lebo ya kurekodi muziki, ninachomiliki tu ni Konde Gang, kundi la watu wawili. Nasubiria wengine wawili Zaidi. Endeleeni kunitegi kwa talanta nzuri na za ajabu. Kwa pamoja acha tushirikiane na tuipeleke kote duniani,” alisema.
Hii inakuja siku chache baada ya uvumi kuibuka kwamba Ibraah hayuko na furaha kuwepo katika lebo hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kufunika kivuli chake kwa takribani miaka 2 sasa.
Ibraah hata hivyo alikanusha madai hayo na kusema kwamba hawezi kuondoka Konde Gang kwani anamuona Harmonize kama baba yake kimuziki.
Kwa upande mwingine, Anjella, msanii aliyewahi kuwa chini ya Harmonize alimpasha wikendi iliyopita baada ya Harmonize kudai kwamba Anjella na wenzake walioondoka walikuwa wakidanganywa kwamba watapata mafanikio Zaidi wakiwa nje ya lebo hiyo.
Alisema kwa kujipiga kifua kwamba haidhuru, yeye kama ‘baba’ alizibariki safari zao na kuwatakia kila la khri.
Anjella akimjibu alisema kwamba Harmonize ndiye aliyekuwa adui mkubwa wa riziki zao na kusema kwamba hakuna safari hata kidogo aliyobariki wakati yeye anaondoka kuwafuata Killy na Cheed.