Wiki moja baada ya kutangaza ujio wa wasanii wengine wawili chini ya lebo ya Konde Gang, Harmonize anazidi kuwapa mashabiki wake viashiria vyote kuhusu utambulisho wa vipaji hivyo vipya vitakavyojiunga naye muda si mrefu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize alipakia msururu wa mazungumzo kwenye DM yake na msanii Hanstone.
Hanstone alipata umaarufu Zaidi mwaka 2019 kufuatia ufanisi mkubwa wa kolabo yake ya ‘iokote’ na Maua Sama.
Tangu kipindi hicho, amekua akiachia ngoma lakini ndio hivyo tena hajakuwa akisikika sana kama ambavyo alisikika kipindi ‘iokote’ ipo katka anga za juu kwenye malimwengu ya muziki.
Harmonize baada ya kuonyesha mazungumzo yao, aliwauliza mashabiki wake ikiwa wataridhia yeye kumchukua kama mrithi wa nafasi iliyoachwa na Anjella aliyetimka mwaka juzi.
Alimtaja Hanstone kama kipaji cha kweli na kuuliza kama itakuwa sawa kwake yeye kuacha kipaji hicho kupotea hivi hivi.
“Can we let really talent die Au tumuunganishe Na Chama Linalo Mtegemea MUNGU, Konde Gang?” Harmonize aliuliza.
Hii inakuja siku mbili tu baada ya Harmonize kuweka wazi kwamba kwa sasa Konde Gang sio lebo bali ni jeshi la watu wawili tu – yeye na Ibraah na kutangaza kwamba ataongeza wengine wawili ili wawe jeshi la watu wanne.
Itakumbukwa Hanstone aliwahi kuhusishwa na kwenda WCB Wasafi kuziba pengo lililoachwa na Rayvanny lakini uvumi huo ukaja kuzima kabla ya Dvoice kutambulishwa kama mrithi halali wa nafasi hiyo.