Andrew Kibe kwa mara ya kwanza amenyoosha maelezo kuhusu uvumi unaoendeshwa katika mitandao ya kijamii kwamba amewahi kuwa mhubiri.
Kibe anamlaumu mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor maarufu Jalang’o kwa kuanzisha uvumi huo ambao kwa upande wake aliutaja kuwa wa uongo.
Hata hivyo, Kibe alipata kibarua kigumu kuzizungumzia picha ambazo zimekuwa zikienezwa mitandaoni zikimuonesha akiwa kanisani kama mhubiri na zingine pia akionekana kuwa na Biblia.
Kwa mujibu wake, hajawahi kuwa mchungaji lakini picha hizo ni wakati alikwenda kwenye mazishi kumwakilisha mhubiri rafiki yake ambaye alikuwa mlevi.
“Mimi sijawahi kuwa pasta, sijawahi kuwa mtu wa kuongoza mazoezi kwenye gym. Lakini kuna siku moja rafiki yangu ambaye ni pasta, alikuwa amelewa kiasi na hangeweza kufanya ibada kwenye mazishi ya mtoto. Kwa hiyo akanipigia simu akaniambia hatuwezi pata mchungaji na unajua lazima tuongoze yale mazishi. Mimi huyo nikavaa suti nikaenda. Natamani ungekuwepo unione kwenye hayo mazishi kwenye makaburi ya Lang’ata,” Kibe alieleza.
“Niliomba hapo, nikatoa mpaka mahubiri. Hata sasa hivi ukitaka naweza hubiri, nilijifunza Biblia kwa sababu rafiki wangu kipindi hicho alikuwa mhubiri,” aliongeza.
Kibe alisema kwamba vitu ambavyo vinaendelea mitandaoni ni vya uongo ambavyo ni vya kumchafua.
Akizungumzia kuondoka nchini ghafla, Kibe alisema kwamba kipindi hicho alikuwa amefilisika pakubwa na alihitaji kupata wazo jinsi ya kujikwamua kifedha.
Hivyo alizungumza na rafiki wake wa Marekani akamwambia kuhusu kila kitu na rafiki huyo akamtumia hela za kufanya nauli ya ndege na hivyo ndivyo aliondoka.