Kwa nini Lilian Ng'ang'a alikasirishwa na mwanadada aliyeketi na mwanaume kando yake

Bi Nganga alionekana kukerwa na tabia ya mwanamke huyo na hakusita kueleza kutoridhika kwake.

Muhtasari

•Lilian Nganga ameibua wasiwasi kuhusu tabia ya watu kutumia simu zao wanapokuwa kwenye kikao maalum na mtu mwingine.

•Alishuhudia mwanadada akitumia simu wakati mwanaume aliyekuwa naye akimuongelesha kwa zaidi ya saa moja.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Mke wa mwanamuziki Juliani, Bi Lilian Nganga ameibua wasiwasi kuhusu tabia ya watu kutumia simu zao wanapokuwa kwenye kikao maalum na mtu mwingine.

Katika taarifa yake ya Jumatano kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa mtoto mmoja wa kiume alisema kuwa tabia hiyo ni ya kukosa heshima na ya kusikitisha huku akiwashauri watu waweke simu zao kando kila mara wanapokuwa wanashiriki mazungumzo na mwingine.

"Kuweka simu chini ukiwa na mtu- katika kikao cha chakula cha mchana, chakula cha jioni n.k- kunaonyesha heshima kwa mtu," Lilian Nganga alisema Jumatano jioni.

Aliendelea kusimulia kisa alichoshuhudia ambapo mwanadada mmoja aliendelea kutumia simu yake wakati mwanaume aliyekuwa naye akizungumza naye kwa zaidi ya saa moja.

"Nimeketi karibu na watu wawili na mwanadada hajaweka simu yake chini (kwa zaidi ya saa moja sasa). Jamaa huyo amekuwa akiongea bila kukoma na mara kwa mara kuna ‘hhmm’ kutoka kwa mwanamke huyo,” alisimulia.

Aliongeza, "Hata ameshikilia simu kwenye glasi ili aweze kupekua vizuri zaidi."

Bi Nganga alionekana kusikitishwa na kukerwa na tabia ya mwanamke huyo na hata alitumia emoji ya uso wenye hasira kuonyesha kutoridhika kwake.