Niko na 'forehead' kubwa na ninaipenda, siifichi- Charlene Ruto ajibu mashambulizi ya mitandaoni

Binti ya Rais William Ruto, Charlene Ruto ameweka wazi kwamba anafahamu kuwa ana paji la uso kubwa.

Muhtasari

•Akizungumza katika mahojiano na Citizen TV, Charlene hata hivyo alibainisha kuwa anapenda paji la uso wake licha ya ukubwa wake.

•Charlene alibainisha kuwa kando na paji lake kubwa la uso, Wakenya pia wamemshambulia kuhusu nywele na mapambo yake.

Charlene Ruto
Binti ya rais William Ruto, Charlene Ruto
Image: HISANI

Binti ya Rais William Ruto, Charlene Ruto ameweka wazi kwamba anafahamu kuwa ana paji la uso kubwa.

Akizungumza katika mahojiano na Victoria Rubadiri kwenye Citizen TV, Charlene hata hivyo alibainisha kuwa anapenda paji la uso wake licha ya ukubwa wake.

 Binti ya rais alitoa maoni hayo wakati akiwajibu wakosoaji wengi wa mwili wake, sura na mitindo.

"Nina paji la uso kubwa na napenda paji la uso wangu. Ninamaanisha, napenda sana paji la uso wangu na siifichi, " Charlene alisema siku ya Jumamosi jioni.

Alibainisha kuwa watu walianza kuuangazia sana mwili na mtindo wake baada ya yeye kupata umaarufu mkubwa mwaka wa 2022 alipozindua ziara za kote nchini.

Binti wa rais alifichua kwamba hata wakati wasaidizi wake wa vyombo vya habari wanauliza kuficha sehemu yake kutokana na wasiwasi, mara nyingi huwaagiza wasifiche chochote.

"Hata wanapoficha kutumia nywele zangu, nawaambia, msifiche paji la uso, lipo na Mungu alinibariki nalo," alisema.

Charlene alibainisha kuwa kando na paji lake kubwa la uso, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii pia wamemshambulia kuhusu nywele na mapambo yake.

Binti ya rais alifichua kuwa kushambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na sura yake kulimfanya ajumuishe unyanyasaji wa mtandaoni miongoni mwa mambo thelathini ambayo anataka kusaidia kukabiliana nayo nchini.

"Tunapopata jukwaa, hatuhitaji kuitumia vibaya. Hebu tuitumie kama jukwaa la kutiana moyo, na kuzungumza vyema kuhusu kila mmoja wetu,” alisema.

Charlene alisema kwamba alianza ziara kote nchini mnamo 2022 ili kuandika hadithi yake mwenyewe kwani watu walikuwa wakipata mawazo yasiyo sahihi juu yake.