Harmonize ajivunia baada ya Alikiba kuzindua media yake, huku Diamond akipuuza

Konde Boy pia alimpongeza mwanamuziki huyo mwenzake kwa miongo miwili ambayo amekuwa kwenye tasnia ya burudani.

Muhtasari

•Konde Boy alichukua hatua ya kumpongeza bosi huyo wa Kings Music Records kwa kuzindua jumba lake la habari, Crown Media.

• Diamond Platnumz ambaye pia anamiliki kituo cha redio na cha Televisheni hata hivyo bado hajampongeza kwa mafanikio hayo.

katika picha ya maktaba.
Alikiba na Harmonize katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worlwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameendelea kuonyesha wazi kuwa hakuna uadui kati yake na staa mwenzake wa bongo fleva Alikiba.

Jumapili jioni, Konde Boy alichukua hatua ya kumpongeza bosi huyo wa Kings Music Records kwa kuzindua jumba lake la habari, Crown Media mnamo siku ya Jumamosi. 

Pia alimpongeza mwanamuziki huyo mwenzake kwa miongo miwili ambayo amekuwa kwenye tasnia ya burudani.

“Nyingine, hongera 👑 , miaka 20.. 📻 📺 ,” Harmonize alimwandikia Alikiba kupitia mtandao wa Instagram. 

Anayeaminika kuwa mshindani mkuu wa Alikiba, Diamond Platnumz ambaye pia anamiliki kituo cha redio na cha Televisheni hata hivyo bado hajampongeza kwa mafanikio hayo. Hata hivyo, hilo lilitarajiwa kwani mastaa hao wawili wa bongo wanaaminika kuwa na uhusiano mbaya kwa miaka mingi.

Alikiba alizindua vituo vyake vya Crown FM na Crown TV Jumamosi jioni wakati akisherehekea miaka ishirini katika tasnia ya burudani.

Huku akizungumzia sababu ya kuamua kuzindua vituo vyake vya habari, staa huyo wa bongo fleva alibainisha kuwa redio na tv zimekuwa nguzo kuu katika kujenga taaluma yake ya muziki.

“Media ni chombo chenye nguvu sana, Media ndio iliyonifanya kuwa Alikiba huyu wa leo,” Alikiba alisema wakati wa uzinduzi wa vituo vyake.

Aliongeza, “Ila pia mimi nilikuwa silali bila redio yangu ndogo niliyoletewa zawadi na baba yangu kupigwa muziki. Changamoto nilizopitia na kutatua kuleta suluhisho kwenye media ndivyo ndivyo vimenipa msukumo."

Mwimbaji huyo mkongwe alitangaza kuwa Crown Media haitakuwa na kituo cha redio na tv pekee, bali pia itakuwa na majukwaa ya kidijitali ili kusaidia kufikia mahali ambapo hakuna mipaka na pia huduma ya usimamizi wa hafla ambayo itasaidia kufika pale mashabiki walipo.

“Crown ipo kwa ajili ya wote ambao wanatafuta majibu ya maswali yao, wanaoutafuta ubora na utofauti pamoja na kasi na huduma,” alisema Kiba.

Alikiba alijiunga na kina Diamond Platnumz na Francis Ciza Majizzo kwenye orodha ya mastaa wa bongo wanaomiliki vyombo vya habari.

Diamond anamiliki Wasafi Media (Wasafi TV, Wasafi Radio) huku Majizzo ambaye pia mcheza santuri akimiliki E-FM na TV-E.