Mike Sonko aguswa na mwanadada aliyemchora kwenye paja, aomba kukutanishwa naye

Bi Njoki alisema kwamba ukarimu wa Sonko ulimvutia na alitaka tu kumshangaza kwa kuchora tattoo hiyo.

Muhtasari

•Bi Njoki alimwomba gavana huyo wa zamani amsaidie akitaja kwamba hayuko katika hali nzuri ya kifedha.

•Sonko aliomba umma kumsaidia kumtafuta mwanadada huyo na kumpeleka ofisini kwake kwa mkutano.

amechora sura ya Mike Sonko kwenye paja.
Bi Mary Njoki amechora sura ya Mike Sonko kwenye paja.
Image: TWITTER

Mfanyibiashara maarufu na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko amemjibu mwanamke kutoka kaunti ya Murang’a ambaye alichora tattoo ya uso wake kwa mguu.

Hii ni baada ya mwanadada aliyejitambulisha kama Mary Njoki kufanya video akiyoonyesha tattoo ya uso wa mwanasiasa huyo ambayo alichora kwenye sehemu ya juu ya paja lake la kushoto.

Katika video hiyo iliyosambazwakwenye mitandao ya kijamii, Bi Njoki alimwomba gavana huyo wa zamani amsaidie akitaja kwamba hayuko katika hali nzuri ya kifedha.

“Hi Sonko, Mike Sonko, Habari yako. Mimi ni Mary Njoki kutoka Murang’a. Mimi ndiye nilikuchora tattoo, na ndiyo hii hapa kwa mguu. Mimi napitia mashida nyingi sana, naomba tu unisaidie. Niko na watoto wanafaa ukubwa. Sina familia, sina wazazi. Ni watoto tu, niko pekee yangu mimi, na naomba tu unipee. Ata kama ni kazi, naomba tu unipe.

Watoto wangu wanataka kukula, kutaka kukunywa na kuomba tu ata kama ni kazi tu utanipea nitafanya, nitashukuru tu Mungu,” Bi Njoki alisema.

Akizungumzia sababu ya kuchora tattoo hiyo, mwanamke huyo alisema kwamba ukarimu wa Sonko ulimvutia na alitaka tu kumshangaza.

“Nakuomba tu Mike Sonko, nisaidie tu. Mungu atakubariki. Ndiye huyu mimi, na ndiyo hii tattoo hapa, mwanadada kutoka Murang’a,” alisema.

Kwa kweli, video ya mwanadada huyo ilifika kwa Mike Sonko na mwanasiasa huyo mtata akajibu kupitia ukurasa wake wa X ambapo alionyesha nia ya kukutana naye.

Katika majibu yake, gavana huyo wa zamani wa Nairobi aliomba umma kumsaidia kumtafuta mwanadada huyo na kumpeleka ofisini kwake kwa mkutano.

“Maskini, nimekutana na video nyingine ya huyu dame aliyenichora tattoo. Whoever knows her amlete kwa office yangu, mnaona nimpe kazi gani?” Sonko aliandika Jumapili jioni.

Picha za tattoo ya Bi Njeri zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii baada ya kupata umarufu kama "Mwanadada wa Murang'a mwenye tattoo ya Mike Sonko."