Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameorodhesha wimbo wa Diamond na Jay Melody ‘Mapoz’ miongoni mwa nyimbo zake tatu bora za bongofleva mwaka 2024.
Konde Boy aliutaja wimbo huo kuwa ni wimbo wake wa tatu bora mwaka huu wakati akikana kuwa msanii wa bongofleva mnamo siku ya Jumapili, Machi 17.
Katika taarifa ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, alileza kuwa yeye si msanii wa bongofleva bali ni shabiki mkubwa wa aina hiyo ya ya muziki.
“Mimi sio msanii wa bongofleva. Mimi ni shabiki namba moja tu wa bongofleva na hii ndio top yangu (3) 2024 1. Dharau ya Ibraah, 2. Daah ya Nandy, 3.Mapozi ya Diamond,” ameandika Harmonize.
Aliendelea kueleza kwa nini yeye si msanii wa bongofleva akiongeza kuwa amekuwa akifanya nyimbo za kiingereza na kufanya kolabo na wasanii wa Kimataifa.
"Niite msanii wa Tanzania au Konde Boy Number One," alisema.
Kauli ya bosi huyo wa Konde Music Worldwide imekuja ikiwa ni wiki moja tu baada ya kupatanishwa na mpinzani wake wa muda mrefu Diamond Platnumz.
Jumatano wiki jana, Harmonize alitoa shukrani kwa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumpa jukwaa la kukutana na bosi wake wa zamani Diamond Platnumz.
Mastaa hao wawili wa bongo fleva ambao wanaaminika kuzozana kwa muda mrefu walikutana katika Ikulu ya Tanzania siku ya Jumanne wiki jana ambapo rais Samia alikuwa amewaalika watu mashuhuri kwa sherehe za Iftar.
Akizungumzia tukio hilo lililowakutanisha mastaa wengi wa bongo, Konde Boy alikiri ilikuwa ni hisia nzuri kukutana na Diamond Platnumz.
“Allah tunakuomba uzipokee fungu zetu , utusamehe makosa yetu kupitia neema ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Asante rais wetu kwa mualiko na kutuweka pamoja vijana wako,” Harmonize aliandika kwenye video yake akimkumbatia Diamond aliyochapisha kwenye Instagram.
Katika video hiyo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alionekana kufurahishwa sana na kuridhishwa sana huku akimkumbatia Diamond kwa nyuma.
“Ilikuwa nzuri kukutana nawe hapa Naseeb. Ramadhan Kareem,” aliandika.
Diamond pia alisherehekea kukutana na msanii huyo wake wa zamani katika WCB na kumtambua rais Samia kwa kuwaleta pamoja.
“Watoto wa mama kizimkazi,” aliandika.
Waimbaji hao wawili ambao wamekuwa wakitawala katika tasnia ya muziki wa bongo fleva kwa miaka kadhaa iliyopita wamekuwa hawana uhusiano mzuri kwa muda mrefu.