Kwa nini nyanya ya Brian Chira anataka azikwe akiwa amevalishwa vazi la kuhitimu

Marehemu mwanatiktok Brian Chira atazikwa Jumanne wiki ijayo, Machi 26.

Muhtasari

•Wakati akitoa mipango hiyo ya maziko, Baba Talisha alifichua kuwa marehemu mwanatiktok huyo atazikwa katika vazi la kuhitimu.

•“Lilikuwa ombi maalum kutoka kwa cucu kwamba Brian akizikwa avalishwe vazi la kuhitimu kwa sababu Brian alikuwa mwanafunzi mwerevu sana," Baba Talisha alisema.

Image: INSTAGRAM// CHIRA BRIAN

Marehemu mwanatiktok wa Kenya Brian Chira atazikwa Jumanne wiki ijayo, Machi 26.

Mwanatiktok Baba Talisha alizungumza Jumatano asubuhi kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya mazishi akifichua kuwa mwanafunzi huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Kabarak atazikwa mahali alikotoka nyanyake.

Ibada ya mazishi kwanza itafanyika katika eneo la Kiarie, Githunguri ambapo nyanya yake marehemu amekuwa akiishi.

“Ibada ya mazishi itakuwa mahali ambapo nyanya yake amekuwa akiishi kwa sababu kuna uwanja mkubwa na watu watafaa. Ni mahali pazuri sana,” Baba Talisha alisema.

Wakati akitoa mipango hiyo ya maziko, Baba Talisha alifichua kuwa marehemu mwanatiktok huyo atazikwa katika vazi la kuhitimu.

Alisema hii itafanywa ili kuheshimu ombi maalum la nyanyake Chira kwani anataka ubingwa wa mjukuu wake darasani utambuliwe.

“Lilikuwa ombi maalum kutoka kwa cucu kwamba Brian akizikwa avalishwe vazi la kuhitimu kwa sababu Brian alikuwa mwanafunzi mwerevu sana. Alipata A-. Hilo lilikuwa ombi maalum kutoka kwa bibi,” alisema.

Baba Talisha alisema waombolezaji kwanza watakusanyika katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa, kabla ya kuelekea kwenye eneo la mazishi.

Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, ikifuatiwa na ibada ndogo ya mazishi kabla ya waombolezaji kuelekea kwenye ibada kuu katika eneo la Githunguri.

“Ataenda kuzikwa mahali nyanya alitoka. Si kila mtu atakayefikia mahali hapo, labda familia ya karibu na watu wachache kama makasisi. Hao wengine watabaki hiyo pande ingine wakikula, penye tutakuwa tukifanyia mazishi,” aliongeza.

Mwanatiktok huyo iliwataarifu mashabiki na wanamitandaoni ambao watataka kuhudhuria mazishi ya Chira kupanga usafiri wao wenyewe akisema atatoa maelekezo.

Brian Chira aliuawa katika ajali ya barabarani mnamo Jumamosi usiku Machi 16, 2024.

Taarifa za kifo cha Chira zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi mchana.

Kulingana na Polisi, Chira alifariki kutokana na ajali aliyohusika nayo katika eneo la Karuri.

Polisi pia walisema kuwa marehemu alikuwa kwenye baa moja eneo la Gacharage na baadaye kusababisha zogo.  Kisha alilazimishwa kutoka.

Baadaye, alichukua pikipiki hadi nyumbani kwake na kushuka kabla ya kujaribu kuvuka kwa miguu.

Lori lililokuwa likienda mwendo kasi lilimgonga na kuondoka kwa kasi. Halikusimama, mashahidi na polisi walisema. Suala hilo liko chini ya uchunguzi.