logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Muigizaji wa Nigeria Amaechi Muonagor alilia msaada baada ya kuzidiwa na ugonjwa wa figo

Muigizaji Kingsley Orji ameeleza kuwa muigizaji huyo mkongwe anasumbuliwa na matatizo ya figo.

image
na Samuel Maina

Burudani20 March 2024 - 07:59

Muhtasari


  • •Bw Muonagor alionekana akiwa dhaifu huku akiwa amelala kitandani aking’ang’ana kuomba msaada wa kifedha ili kupandikizwa figo.
  • •Muigizaji Kingsley Orji ameeleza kuwa muigizaji huyo mkongwe anasumbuliwa na matatizo ya figo.
anapambana na ugonjwa wa figo.

Muigizaji mkongwe wa Nigeria Amaechi Muonagor amejitokeza kuomba msaada wa kifedha baada ya afya yake kudorora.

Video inayomuonyesha muigizaji huyo mkongwe akiwa dhaifu huku akiwa amelala kitandani aking’ang’ana kuomba msaada wa kifedha ili kupandikizwa figo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii katika siku chache zilizopita.

Katika video hiyo, muigizaji huyo anaonekana akiwa amevimba usoni na bandeji kifuani huku akijaribu sana kueleza hali yake na kuomba msaada.

"Watu wa Igbo, nawasalimu nyote," Muonagor anasikika akisema kwa lugha ya Igbo kabla ya kushindwa kuzungumza zaidi.

Baada ya kushindwa kuendelea kuzungumza, muigizaji mwingine, Kingsley Orji anachukua nafasi akieleza kuwa msanii huyo mkongwe anasumbuliwa na matatizo ya figo.

"Haijakuwa rahisi. Amekuwa katika hali hii kwa miezi sasa, Anataka kwenda kupandikizwa figo," muigizaji Orji alieleza.

Aliendelea, "Amerudi kutoka ICU, siku kadhaa zilizopita. Alikuwa akipokea matibabu lakini sio vizuri. Tuliamua kumrudisha nyumbani kwa sababu hakukuwa na pesa lakini haifai, anazungumza vizuri. Tafadhali, anahitaji msaada wako.”

Muigizaji mwingine, aliyeketi karibu naye, anaendelea kulezea kwamba Muonagor anahitaji pesa kulipia upandikizaji wa figo nchini India.

Habari kuhusu ugonjwa wa Bw Muonagor zinajiri wiki chache tu baada ya kifo cha muigizaji mwenzake mkongwe John Okafor almaarufu Mr Ibu.

Mr Ibu alifariki kutokana na mshtuko wa moyo mnamo Machi 2, 2024.

Mchekeshaji huyo alikata roho katika Hospitali ya Evercare nchini Nigeria siku ya Jumamosi, akiripotiwa kufariki dunia akiwa katika hali ya kukosa fahamu.

Matatizo ya afya ya Bw Ibu yalijulikana kwa umma Oktoba mwaka jana wakati familia yake iliposambaza video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha nyota huyo wa Nollywood akisherehekea siku ya kuzaliwa kutoka kwa kitanda chake hospitalini.

Katika video hiyo, aliwaomba mashabiki wake usaidizi wa bili za matibabu, na kusababisha uungwaji mkono mkubwa.

Katika ombi lake, alisema, "Wapendwa watu wema wa Nigeria, tunategemea msaada wenu wakati huu tunapouhitaji zaidi... Ninapozungumza na wewe, bado nimelazwa hospitalini; mkurugenzi wa matibabu wa hospitali hii alisema kuwa suluhu bora zaidi ni, ikiwa wazo lake jipya halitafanya kazi, wazo bora ni kukata mguu wangu."


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved