RIP! Mzee aliyebuni msemo maarufu 'kata simu tupo site' afariki dunia

Mchekeshaji mkongwe wa Tanzania Umar Iahbedi Issa almaarufu Mzee Mjegeje amefariki dunia.

Muhtasari

•Mzee Mjegeje alikata roho Jumatano asubuhi katika Hospitali ya Mwananyamala iliyo Dar es Salaam, Tanzania alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mzee Mjegeje
Image: HISANI

Mchekeshaji mkongwe wa Tanzania Umar Iahbedi Issa almaarufu Mzee Mjegeje amefariki dunia.

Mzee Mjegeje ambaye alifahamika zaidi kwa video yake ya vichekesho "Kata simu tupo site" alikata roho siku ya Jumatano asubuhi katika Hospitali ya Mwananyamala, iliyo Dar es Salaam, Tanzania alikokuwa akipatiwa matibabu.

Meneja wa mchekeshaji huyo, Real Jimmy alithibitisha habari hizo za kusikitisha lakini hakufichua ugonjwa uliosababisha kifo chake.

Mzee Mjegeje ambaye pia alijitambulisha kwa jina la Raisi wa Bagamoyo alikuwa mkazi wa eneo la Bagamoyo katika mkoa wa Pwani, nchini Tanzania.

Alipata umaarufu wa kimataifa hata nchini Kenya mwaka wa 2022 wakati video yake “kata simu, tupo site” ilipovuma sana kwenye mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo iliyomzolea umaarufu mkubwa, msanii huyo wa vichekesho alionekana akiongea kwenye simu ndogo akisema, "Kata simu, kata simu, tupo site. We don't like disturbance of the head you understand. "

Maneno ya mchekeshaji huyo kwenye video hiyo tangu wakati huo yamekuwa yakitumika katika meme nyingi na hata baadhi ya wasanii wengine wameyatumia kwenye nyimbo zao.

Roho ya Mzee Mjeje ipumzike pema peponi!!!