“Huwa nalia nikitamani ungekuwa hapa!” Nazizi ashiriki kumbukumbu yake maalum na marehemu mwanawe

Alionyesha video yake akilia huku akitazama picha ya marehemu mwanawe iliyowekwa ukutani.

Muhtasari

•Jazeel alipoteza maisha mnamo siku ya Krismasi mwaka jana kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli moja nchini Tanzania.

•"Sasa umeenda kijana wangu, mama hana mtu wa kukaa naye jioni na mimi hulia na kulia nikitamani ungekuwa hapa," alisema.

Image: INSTAGRAM// NAZIZI

Rapa mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji, mnamo Jumatano jioni alikumbuka kihisia kumbukumbu zake na marehemu mtoto wake Jazeel Adam.

Mwanawe Nazizi mwenye umri wa miaka mitatu alipoteza maisha mnamo siku ya Krismasi mwaka jana kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli moja nchini Tanzania.

Katika chapisho la hisia siku ya Jumatano, mwimbaji huyo mzaliwa wa pwani alikumbuka jinsi alikuwa akitumia jioni zake na mvulana huyo mdogo, wakitazama programu ya watoto, kucheka pamoja na kukumbatiana. Alitaja nyakati za jioni kuwa nyakati alizopenda zaidi kwa siku.

"Ilikuwa wakati wangu niliopenda sana kwa siku ambapo tulipumzika na kutazama paw patrol na kucheka na kukumbatiana," Nazizi aliandika kwenye Instagram.

Nazizi aliambatanisha ujumbe wake na video fupi iliyoonyesha akilia huku akitazama picha ya marehemu mwanawe iliyowekwa ukutani.

Aliendelea kufunguka jinsi anavyomkosa mwanae, na jinsi anavyolia kila jioni akikumbuka kuwa mtoto huyo hayupo naye tena.

"Sasa umeenda kijana wangu, mama hana mtu wa kukaa naye jioni na mimi hulia na kulia nikitamani ungekuwa hapa," alisema.

Mapema mwezi huu, msanii huyo alidokeza kuwa ametumia takriban miezi miwili na nusu iliyopita akiwa amejifungia ndani ya nyumba yake kufuatia kifo cha mwanawe.

Katika taarifa yake, mwimbaji huyo wa kundi la Necessary Noize aliwashukuru wale ambao wamekuwa wakimtia moyo kuondoka nyumbani na kuungana tena na ulimwengu lakini akadokeza kuwa haijakuwa rahisi kwake tangu mwisho wa mwaka jana.

"Kwa kila mtu anayenitia moyo nitoke nyumbani.. asante lakini, imepita miezi 2 na nusu ya vita hivi..," Nazizi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha ujumbe wake na meme inayoelezea jinsi wakati mwingine anahisi huzuni sana kuondoka nyumbani na nyakati nyingine anahisi kuondoka nyumbani kunaweza kupunguza huzuni yake.

"Vita kwenye ubongo.. Kuhisi huzuni sana kuondoka nyumbani ... Kujua kwamba kwenda nje kutafanya nihisi huzuni imeshuka chini," meme aliyoposti ilisema.

Mwimbaji huyo  pia aliweka chapisho la kutia wasiwasi wakati akiendelea kuomboleza mwanawe aliyeaga siku ya Krismasi.

"Kwa sababu za kibinafsi, nitakuwa naomboleza leo, kwa sababu watu ninaowapenda waliokufa bado wamekufa sana," posti aliyoweka ilisomeka.