Mkewe Pasta Ezekiel awataka wanawake kutowasukuma waume kujenga nyumba vijijini

"Hatuna nyumba kule nimeolewa. Tukifika huko gari ndio nyumba yetu. Pastor Ezekiel ndio firstborn na sijalilia nyumba", alisema.

Muhtasari
  • Hapo awali, Mchungaji Sarah alizungumza kuhusu ndoa, akiwashauri wanawake kuwa waombaji ili mahusiano yao yadumu.
Mke wa pastor Ezekiel, Sarah Wanzu.
Image: Hisani

Mke wa Mchungaji Ezekiel, Sarah Wanzu amefunguka kuwa hana nyumba kijijini  na wanawake waache kuwasukuma waume zao kujenga nyumba.

Akiongea katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la New Life eneo la Mavueni kaunti ya Kilifi, mama huyo wa watoto watatu alisema ndoa sio tu kujenga nyumba yako mwenyewe.

"Hatuna nyumba kule nimeolewa. Tukifika huko gari ndio nyumba yetu. Pastor Ezekiel ndio firstborn na sijalilia nyumba", alisema.

Aliwataka wanawake wanaolalamikia waume zao kutowajengea nyumba kuacha na kuzingatia mambo ya maana.

"Nyumba sio ndoa na nyumba sio maisha. Mimi sijajengewa. Na ukijengewa na ukaachwa, hio nyumba nani atakaa hapo", alieleza.

Mhubiri huyo alisema anachotaka ni maisha yenye afya na nguvu zaidi za kumtumikia Bwana. Sarah alisema licha ya kuwa hajamaliza shule, anataka kuhubiri injili ya Mungu duniani kote.

Hapo awali, Mchungaji Sarah alizungumza kuhusu ndoa, akiwashauri wanawake kuwa waombaji ili mahusiano yao yadumu.

Mume wa Sarah pastor Ezekiel alifichua kwamba hakuwa na siri na anashiriki kila kitu na mke wake.

Alisema mkewe anajua PIN yake ya pesa za rununu na pia ana ufikiaji kamili wa simu zake.

Mhubiri huyo alifichua kuwa ndoa yao haikuwa kamilifu na alipendelea kusuluhisha maswala ya uhusiano wao ndani ya chumba chao cha kulala kuliko kuhusisha watu wengine.