Mzalishaji wa muziki wa Gengetone, Magix Enga ameonesha hisia zake baada ya kugundua video katika jukwaa la video la YouTube ikiwa inamzungumzia kama mfu.
Akizungumza kwenye podikasti ya Mseto East Africa, Enga alisema kwamba watu wengi walikuwa wamejua ameshaisha baada ya kukumbwa na matatizo ya msongo wa mawazo.
Alisema kwamba aliumia sana kuona mtu anafanya video ya kumtakia ‘pumziko la amani’ kwenye YouTube ili tu kutafuta umaarufu, wakati yeye yuko hai na mzima wa afya.
“Hata sai kuna video nimeona YouTube imeandikwa ‘RIP’, nimeonyesha rafiki yangu hapa asubuhi, inasema ‘RIP Magix Enga’ unaweza tafakari…” Enga alisema huku akijaribu kuzuia machozi.
“Eeeh si rahisi, kwa sababu sasa unaweza fikiria kuna watoto wako nyumbani, wanaona wanashangaa tena eti RIP tena,” aliongeza.
Akitoa ujumbe kwa watu ambao walijua chake kimekwisha, Enga alisema;
“Mimi naweza waambia Mungu ndiye kila kitu. Sasa hivi niko sehemu nzuri na ningependa watu wote walioko mtaa duni niliokuwa watoke hapo na kuwa sehemu nipo sasa hivi.”
Akizungumzia chimbuko la msongo wa mawazo ambao ulimporomosha pakubwa, Magix Enga alisema yote yalianza wakati matapeli walikuwa wanalaghai watu kwa kutumia ukurasa wake wa Facebook.
Enga alisema kwamba watapeli walikuwa wanaibia watu Facebook kwa kuwahadaa watume pesa ili wapate muda wa kurekodi ngoma kisha wakishatumiwa pesa, wanawapa namba yake [Enga] ili kumpigia wakifuatilia ahadi hiyo.
Enga alikuwa anashangaa kupokea simu akiambiwa ametumiwa pesa kumbe zilikuwa zinatumwa kwa namba tofauti kisha ya kupigiwa simu inakuwa yake, hilo lilimpa msongo wa mawazo hadi akaripoti katika vituo vya polisi Nairobi na Nakuru.