logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mashabiki wachanga zaidi ya milioni 5 katika siku mbili ili kumjengea nyumba nyanyake Brian Chira

Wanamitandao wana mpango wa kumjengea nyanyake Chira nyumba ya vyumba viwili vya kulala kutumia pesa ambazo zitachangwa.

image
na Samuel Maina

Burudani22 March 2024 - 07:38

Muhtasari


  • •Mwanatiktok Baba Talisha alifichua kuwa Sh5,007,799 zilichangishwa kufikia Alhamisi usiku kupitia Paybill 8056605.
  • •Wanamitandao wana mpango wa kumjengea nyanyake Chira nyumba ya vyumba viwili vya kulala kutumia pesa ambazo zitachangwa.
Brian Chira

Jamii ya mitandaoni, hasa watumiaji wa tiktok wameendelea kuchanga kwa moyo mkunjufu  kwa ajili ya mipango ya mazishi ya marehemu Brian Chira.

Mwanatiktok Baba Talisha amewaongoza wanamtandao wenzake kuchangisha pesa, huku jumla ya pesa iliyopatikana kufikia Alhamisi usiku ikifikia zaidi ya Sh5milioni.

Katika taarifa yake la hivi punde Alhamisi usiku, mwanatiktok huyo ambaye ni sehemu ya kamati ya kuandaa mazishi ya Brian Chira alifichua kuwa Sh5,007,799 zilichangishwa kupitia Paybill 8056605. Hii ilikuwa takriban saa 48 baada ya akaunti ya kuchangisha pesa kufunguliwa.

Katika sasisho lingine, Baba Talisha alifichua kuwa wana mpango wa kumjengea nyanyake Chira nyumba ya vyumba viwili vya kulala kutumia pesa ambazo zitachangwa, kwani ilikuwa ni matakwa ya marehemu kumzawadia mlezi huyo nyumba.

“Inafanyika. Wakati ufaao, mimi, Bwana, nitafanya. Isaya 60:22,” Baba Talisha aliandika kwenye video ya kumbukumbu ya Chira akizungumzia kumjengea nyanyake nyumba.

Hapo awali, mtumiaji mwingine wa tiktok alikuwa amejitolea kusimamia gharama yote ya mazishi ya Chira inayofikia zaidi ya Sh800,000. Mwimbaji KRG the Don pia alikuwa amewezesha kuhamishwa kwa mwili wake hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta, na kuahidi kuwa sehemu ya mipango ya maziko.

Mapema wiki hii, kamati ya kuandaa mazishi ilitangaza kwamba mwili wa mwanatiktok Brian Chira utazikwa siku ya Jumanne, Machi 26.

Mwanatiktok Baba Talisha, ambaye ni sehemu ya waandalizi wa mazishi amefichua kuwa mwanafunzi huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Kabarak atazikwa nyumbani kwa nyanyake baada ya ibada ya mazishi kufanyika katika eneo ambapo mlezi huyo amekuwa akiishi Githunguri, kaunti ya Kiambu.

“Ibada itakuwa mahali ambapo nyanya yake amekuwa akiishi kwa sababu kuna uwanja mkubwa na watu watatoshea. Ni mahali pazuri sana, mtaona,” Baba Talisha alisema.

Alisema waombolezaji kwanza watakusanyika katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa, kabla ya kuelekea kwenye eneo la mazishi.

Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, ikifuatiwa na ibada ndogo ya mazishi kabla ya waombolezaji kuelekea kwenye ibada kuu katika eneo la Githunguri.

“Ataenda kuzikwa mahali nyanya alitoka. Si kila mtu atakayefikia mahali hapo, labda familia ya karibu na watu wachache kama makasisi. Hao wengine watabaki hiyo pande ingine wakikula, penye tutakuwa tukifanyia mazishi,” aliongeza.

Mwanatiktok huyo iliwataarifu mashabiki na wanamitandaoni ambao watataka kuhudhuria mazishi ya Chira kupanga usafiri wao wenyewe akisema atatoa maelekezo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved