Wanamitandao waonyesha ukarimu huku wakichanga zaidi ya 7.3m kusaidia familia ya Brian Chira

Zaidi ya shilingi milioni 7 zilikuwa zimekusanywa katika siku ya tatu ya uchangishaji wa mtandaoni.

Muhtasari

•Pesa zilizokusanywa kwa ajili ya mazishi ya mwanatiktok Brian Chira zilifikia zaidi ya Sh7.3m katika siku ya tatu.

•Waandalizi wa harambee hiyo wamedokeza kwamba watatumia fedha hizo kumjengea nyumba nyanya ya marehemu.

Mwanatiktok Brian Chira
Image: RADIO JAMBO

Pesa zilizokusanywa kwa ajili ya mazishi ya mwanatiktok Brian Chira zilifikia zaidi ya Sh7.3m katika siku ya tatu ya uchangishaji wa mtandaoni unaoendeshwa kwenye mitandao ya kijamii

Tiktoker Baba Talisha, anayeongoza uchangishaji huo, mnamo usiku wa kuamkia Jumamosi alifichua kuwa Sh7,330,854 zilikuwa zimekusanywa kufikia wakati huo. Uchangishaji bado unaendelea kupitia paybill 8056605 #Brian.

Marafiki, mashabiki na watumizi wa mitandao ya kijamii wameonyesha ukarimu mkubwa ndani ya takribani siku tatu zilizopita tangu akaunti ilipofunguliwa kusaidia familia ya marehemu Chira. Waandalizi wa harambee hiyo wamedokeza kwamba watatumia fedha hizo kumjengea nyumba nyanya ya marehemu, kwani tayari kuna watu wamejitolea kusimamia gharama za mazishi.

Katika taarifa ya Alhamisi usiku, mwanatiktok Baba Talisha alifichua kuwa Sh5,007,799 zilikuwa zimekusanywa kufikia wakati huo. Hii ilikuwa takriban saa 48 baada ya akaunti ya kuchangisha pesa kufunguliwa.

Katika sasisho lingine, alifichua kuwa wana mpango wa kumjengea nyanyake Chira nyumba ya vyumba viwili vya kulala kutumia pesa ambazo zitachangwa, kwani ilikuwa ni matakwa ya marehemu kumzawadia mlezi huyo nyumba.

“Inafanyika. Wakati ufaao, mimi, Bwana, nitafanya. Isaya 60:22,” Baba Talisha aliandika kwenye video ya kumbukumbu ya Chira akizungumzia kumjengea nyanyake nyumba.

Hapo awali, mtumiaji mwingine wa tiktok alikuwa amejitolea kusimamia gharama yote ya mazishi ya Chira inayofikia zaidi ya Sh800,000. Mwimbaji KRG the Don pia alikuwa amewezesha kuhamishwa kwa mwili wake hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta, na kuahidi kuwa sehemu ya mipango ya maziko.

Mapema wiki hii, kamati ya kuandaa mazishi ilitangaza kwamba mwili wa mwanatiktok Brian Chira utazikwa siku ya Jumanne, Machi 26.

Baba Talisha alichua kuwa mwanafunzi huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Kabarak atazikwa nyumbani kwa nyanyake baada ya ibada ya mazishi kufanyika katika eneo ambapo mlezi huyo amekuwa akiishi Githunguri, kaunti ya Kiambu.

“Ibada itakuwa mahali ambapo nyanya yake amekuwa akiishi kwa sababu kuna uwanja mkubwa na watu watatoshea. Ni mahali pazuri sana, mtaona,” Baba Talisha alisema.

Alisema waombolezaji kwanza watakusanyika katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa, kabla ya kuelekea kwenye eneo la mazishi.

Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, ikifuatiwa na ibada ndogo ya mazishi kabla ya waombolezaji kuelekea kwenye ibada kuu katika eneo la Githunguri.