Gauni ambalo Brian Chira atavalishwa akizikwa, jeneza zanunuliwa huku siku ya mazishi ikikaribia

Marehemu Chira atavalishwa suti kisha gauni la kuhitimu juu yake kama alivyoagiza nyanya yake.

Muhtasari

•Baba Talisha alionyesha suti ambayo marehemu atavalishwa na gauni la kuhitimu ambalo atavalishwa juu, hii ni kutimiza matakwa ya nyanya ya Chira.

•Marehemu atazikwa Jumanne, Machi 26 katika kijiji cha Ingitei-Gathanje, eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

ya mazishi ya Brian Chira inaendelea
Mipango ya mazishi ya Brian Chira inaendelea
Image: HISANI

Huku zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya mazishi ya mwanatiktok Brian Chira, maandalizi ya hafla hiyo tayari yameango’a nanga.

Siku ya Jumamosi, mwanatiktok Baba Talisha ambaye ni sehemu ya kamati ya maandalizi ya mazishi alifichua kuwa nguo ambazo Chira atavalishwa mnamo siku ya mazishi  tayari zimenunuliwa. Alionyesha suti ambayo marehemu atavalshwa na gauni la kuhitimu atakalovalishwa juu ya suti, hii ni kutimiza matakwa ya nyanya ya Chira.

“Tushamaliza kununua gauni, iko hapa. Suti iko hapa. Suti iko pale na viatu, hizo vitu zote zenye mwanaume anafaa kwa mwili. Gauni iko hapa, tushamalizana na matakwa ya shosho,” Baba Talisha alisema kwenye video aliyoshiriki kwenye Tiktok.

Katika chapisho lingine, tiktoker huyo alichapisha video iliyomuonyesha akiwa na nyanyake Chira wakikagua jeneza na kufichua kuwa mwanamuziki KRG the Don tayari alikuwa amelipia jeneza ambalo marehemu atazikwa ndani yake.

"KRG the Don alilipa 32k kwa jeneza kama alivyoahidi na nikaongeza 23k yangu ili kutimiza matakwa ya shosh. KRG sasa atamaliza bili ya chumba cha maiti Jumatatu. Asante,” alisema.

Brian Chira alipoteza maisha baada ya kugongwa na lori kwenye barabara ya Kimbu mnamo Machi 16, 2024.

Atazikwa Jumanne, Machi 26 katika kijiji cha Ingitei-Gathanje, eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

Hapo awali, Baba Talisha alisema waombolezaji kwanza watakusanyika katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa, kabla ya kuelekea kwenye eneo la mazishi.

Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, ikifuatiwa na ibada ndogo ya mazishi kabla ya waombolezaji kuelekea kwenye ibada kuu katika eneo la Githunguri.