Aliyekuwa mtangazaji wa Citizen TV Kimani Mbugua ameomba usaidizi wa kutafuta simu yake baada ya kudaiwa kuibiwa moja kwa moja kwenye TikTok.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, Kimani alidai alivamiwa na mwizi mmoja aliyekuwa amebeba silaha ambapo alipata majeraha ya mguu na mkono.
Alisema alikuwa akitembea kwa miguu huku akirekodi video ya tiktok wakati mshambuliaji huyo alipomwibia.
"Jamani nilivamiwa asubuhi ya leo nilipokuwa live kwenye Tiktok na mvulana aliyekuwa na panga, nilikuwa katika matembezi yangu ya asubuhi katika eneo la Jomoko Thika. Niliumia mguu na mkono lakini ninaendelea vizuri," Kimani aliandika.
Alisema alipoteza simu yake na tayari ameandikisha taarifa katika kituo cha polisi ambao sasa amewaomba usaidizi.
"Niliripoti kesi katika kituo cha polisi cha Kiandu OB no 05/23/03/24. Ninaendelea vizuri lakini nilipoteza Samsung A34 yangu ambayo nyie mlininunulia, nilikuwa naizalisha, polisi wa Kenya naomba mnisaidie kuirejesha tafadhali," aliongeza.
Video ya tiktok inamuonyesha mtangazaji huyo wa zamani wa TV akirekodi moja kwa moja kabla ya jamaa ambaye alionekana kuwa na kisu mkononi kutoka nyuma na kuchukua simu yake.
“Nimefurahi sana pia kurudi,” Kimani alisikika akisema kabla ya simu yake kuchukuliwa.
Takriban miezi mitano iliyopita, Kimani alilezea furaha ayake baada ya kununua kamera na vifaa vya video kupitia mchango aliopokea kutoka kwa wasamaria wema.
Awali alikuwa ametoa ombi la takriban 200,000 ili kuanzisha kampuni yake ambayo alitumai ingemtoa kwenye matatizo.
Kupitia video ya TikTok, aliwashukuru Wakenya wote ambao walisimama na yeye wakati alipokuwa akipitia hali ngumu.
"Nataka kurudi kwako na kusema asante kwa usaidizi wote na upendo wenu, haswa hapa kwenye TikTok," alisema.
Alieleza kwamba alitumia pesa kwa njia mwafaka kwa kununua vifaa ambavyo vingemwezesha kuendeleza shughuli zake za mawasiliano.
"Nimefurahi sana, unaweza kuona usoni mwangu, nina furaha sana, na nilitaka tu kusema asante kwa kila mmoja wenu aliyenipa kiasi chochote cha pesa alichofanikiwa nacho," aliongeza mwanahabari huyo.