Mkali wa rap Khaligraph Jones amedokeza kwamba si muda wote anafurahia maisha ya kushiriki mazoezi ya kunyanyua vyuma kwenye gym kila uchao.
Kupitia insta story, Khaligraph alipakia video akiwa ameketi kwa kujikunyata kwenye gym akionekana kuwa kwenye lindi la mawazo na kusema kwamba wakati mwingine maisha ya gym huwa yanachosha sana.
Jones ambaye kando na weledi wake katika kutema mistari anajulikana na mwili wake uliochongeka kwa mapande sita kutokana na bidii katika kunyanyua vyuma, alionekana kudokeza kuchoshwa na maisha hayo kwa kutumia kauli ya kujipa moyo kwamba ‘kuna miili mipya mbinguni’.
“Hii gym wakati mwingine inachosha sana, ama Mungu atatupa miili mipya mbinguni?” Jones aliuliza.
Hata hivyo, Jones katika klipu ilifuata, alipakia video akionekana kuchangamka akijishaua shaua na kusema kwamba baada ya kushiriki mazoezi kwa muda mchache, mwili wake ulipata kuitikia mazoezi hayo.
“Mwili umechangamka sasa,” Jones aliandika.
Msanii huyo amekuwa akizungumziwa katika vyombo vya habari za burudani kutokana na jumba kubwa la kifahari ambalo analijenga.
Jones alionekana kukumbatia jina la ‘Zetech’ kwa ajili ya jumba hilo ambalo baadhi ya Wakenya walilifananisha na muonekano wa chuo cha Zetech.
Akizungumza katika mahojiano ya awali, Jones alisema kwamba aliona kejeli hizo kaitka mitandao ya kijamii na kusema kwamba kauli kama hizo kuhusu mradi wake hazimbabaishi kwani anataka kuonesha watu kwamba usanii unalipa licha ya wengi kudai kwamba Sanaa ya muziki wa Kenya imedidimia.