Mwanatiktok maarufu wa Kenya Brian Chira anatarajiwa kuzikwa leo, Jumanne, Machi 26 katika eneo la Githunguri, kaunti ya Kiambu.
Chira aliaga dunia mnamo Machi 16, 2024 baada ya kugongwa na lori kwenye barabara ya Kiambu alipokuwa akienda nyumbani kutoka eneo la burudani.
Tangazo la kifo na mazishi ambalo lilitolewa na familia siku chache zilizopita lilionyesha kuwa mwili wa marehemu utaondoka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta Jumanne asubuhi kisha mazishi kufanyika katika kijiji cha Ingitei, Gathanje, eneo la Githunguri, Kiambu.
Mapema wiki iliyopita, mwanatiktok Baba Talisha ambaye ni sehemu ya kamati ya kuandaa mazishi alifichua kuwa mahali ambapo marehemu Chira atazikwa ni yumbani kwa nyanyake.
“Ibada itakuwa mahali ambapo nyanya yake amekuwa akiishi kwa sababu kuna uwanja mkubwa na watu watatoshea. Ni mahali pazuri sana, mtaona,” Baba Talisha alisema.
Alisema waombolezaji kwanza watakusanyika katika Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi kabla ya kuelekea kwenye eneo la mazishi.
Shughuli ya kutazama mwili itafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti, ikifuatiwa na ibada ndogo ya mazishi kabla ya waombolezaji kuelekea kwenye ibada kuu katika eneo la Githunguri.
“Ataenda kuzikwa mahali nyanya alitoka. Si kila mtu atakayefikia mahali hapo, labda familia ya karibu na watu wachache kama makasisi. Hao wengine watabaki hiyo pande ingine wakikula, penye tutakuwa tukifanyia mazishi,” aliongeza.
Jumamosi, Baba Talisha alitangaza kuwa nguo ambazo marehemu Chira angevalishwa mnamo siku ya mazishi tayari zilikuwa zimenunulia.
Alionyesha suti ambayo marehemu angevalshwa na gauni la kuhitimu la kuvalishwa juu ya suti, hii ilikuwa ni kutimiza matakwa ya nyanya ya Chira.
“Tushamaliza kununua gauni, iko hapa. Suti iko hapa. Suti iko pale na viatu, hizo vitu zote zenye mwanaume anafaa kwa mwili. Gauni iko hapa, tushamalizana na matakwa ya shosho,” Baba Talisha alisema.
Katika chapisho lingine, tiktoker huyo alichapisha video iliyomuonyesha akiwa na nyanyake Chira wakikagua jeneza na kufichua kuwa mwanamuziki KRG the Don tayari alikuwa amelipia jeneza ambalo marehemu angezikwa ndani yake.
"KRG the Don alilipa 32k kwa jeneza kama alivyoahidi na nikaongeza 23k yangu ili kutimiza matakwa ya shosh. KRG sasa atamaliza bili ya chumba cha maiti Jumatatu. Asante,” alisema.
Katika taarifa nyingine, mwanatiktok huyo aliomba amani kudumishwa na kutangaza kuwa walevi hawataruhusiwa kwenye hafla ya mazishi.