Mbunge Salasya amwaga maelfu ya pesa katika mazishi ya Brian Chira, afunguka alivyomtia msukumo

Salasya alipewa fursa ya kuhutubia waombolezaji ambapo alimsifu marehemu kwa ufasaha wake wa kuzungumza.

Muhtasari

•Salasya alisifu ushawishi wa Brian Chira kwa kizazi kipya akisema kwamba tiktoker ya umri wa miaka 23 iliwahimiza vijana wengi.

•Aliahdii kumwachia nyanyake Chira Sh 40, 000 kwa matumizi binafsi na pia kusapoti mradi wa nyumba.

alitoa maelfu ya pesa kusaidia familia ya Brian Chira
Mbunge Peter Salasya alitoa maelfu ya pesa kusaidia familia ya Brian Chira
Image: INSTAGRAM// PETER SALASYA

Mbunge wa eneo la Mumias Mashariki Peter Kalerwa Salasya mnamo Jumanne aliwasisimua waombolezaji baada ya kutoa pesa taslimu kusaidia familia ya Brian Chira.

Mwanasiasa huyo kijana alikuwa miongoni mwa maelfu ya waombolezaji waliokuwepo wakati wa mazishi ya marehemu Chira katika eneo la Githunguri, kaunti ya Kiambu.

Alipewa fursa ya kuhutubia waombolezaji ambapo alitumia fursa hiyo kumsifu marehemu kwa ufasaha wake wa kuzungumza.

“Mimi nikiwa hapa naitwa Peter Salasya ambaye ni mbunge wa kule Mumias Mashariki. Niko hapa kwa sababu mimi ni memba mkubwa kule tiktok, na kwa sababu pia mimi huyu Chira amekuwa one of my insipirational speakers kwa kuwa anajua kuongea. Anajua jinsi ya kuongea, nilimjua kupitia mitandao ya kijamii,” Mbunge Salasya alisema.

Aliendelea kusifu ushawishi wa Brian Chira kwa kizazi kipya akisema kwamba tiktoker ya umri wa miaka 23 iliwahimiza vijana wengi.

“Na huyu Chira amekuwa msukumo mkubwa sana kwa kizazi kipya. Na mkiangalia hapa, hakuna mwanasiasa hata mmoja ambaye anaweza vuta vijana ambao mnaona hapa leo. Wale watu ambao nimeona hapa leo sijaamini macho yangu, n ani kwa sababu ya ule ushawishi ambao ndugu yetu amekuwa nao,” alisema.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alisema alihudhuria maziko hayo sio tu kwa ajili ya kumuomboleza marehemu Chira, bali pia kumfariji nyanyake aliyemlea.

"Mimi leo nimekuwa kule Western na nikasema kabla niende kwa kitu chochote, lazima nikuje hapa leo nikulete pole zetu kwa mama ambaye amekuwa mama shosh, ambvaye amemlea," alisema.

Aliitaka roho ya marehemu tiktoker huyo ipumzike kwa amani.

Katika kumsapoti nyanyake Chira, aliahidi kumwachia Sh 40, 000 kwa matumizi binafsi na pia kusapoti mradi wa nyumba ambayo wanamtandao wamepanga kumjengea.

“Mimi nataka nimwambie mama shosh kwamba, mimi kama mheshimiwa mbunge, najua tutaongea na mheshimiwa Wamuchomba, yuko hapa, nitaongea na yeye tuone vile tunaweza kusaidia. Lakini kwa sababu mimi nimefika hapa, nitaacha mchango wangu wa shilingi elfu arobaine ambayo itakusaidia pia kufanya mambo yako,” alisema.

Aliongeza, “Alafu niliskia mama anataka kujengewa, kama kutakuwa na ile programme, I will be there to support. Kama ni kiti, kama ni kitanda, tutaleta."

Baada ya hotuba yake, mbunge huyo alionekana akimkabidhi Baba Talisha noti kadhaa za shilingi elfu moja ili amkabidhi bibi yake Chira.