Marehemu Brian Chira atambuliwa katika seneti, seneta atumia kifo chake kuwatahadharisha vijana

Seneta huyo wa UDA alichukua fursa kumuomboleza Chira na kuwashauri vijana kuwa makini na maisha yao.

Muhtasari

•Seneta Samson Cherargei  alituma risala zake za rambirambi kwa familia ya Brian Chira wakati tiktoker huyo alikuwa akizikwa Kiambu.

•"Ninawaomba vijana kuwajibika katika maisha yao, na kuwa makini. Hasa unapoenda kujivinjari  jijini na mijini," alisema.

alizikwa Jumanne, Machi 26, 2024.
Marehemu Brian Chira alizikwa Jumanne, Machi 26, 2024.
Image: HISANI

Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei mnamo Jumanne alituma risala zake za rambirambi kwa familia ya Brian Chira wakati mtumbuizaji huyo wa tiktok alikuwa akizikwa nyumbani kwa nyanyake katika eneo la Githunguri, kaunti ya Kiambu.

Seneta huyo wa UDA alikuwa amemaliza tu kuunga mkono mswada uliopelekwa katika seneti na seneta wa Homa Bay Moses Kajwang' alipochukua nafasi kuomboleza kifo cha kijana huyo wa miaka 23 na kufariji familia yake.

"Bwana spika, pamoja na matamshi hayo mengi, nataka kuunga mkono mswada huu na pia kuwahakikishia Wakenya kwamba tutafanya yote ambayo ni muhimu kufanywa, na kuruhusu taifa hili kusonga mbele. Pia nataka kutuma salamu zangu za rambirambi Bw Spika, kuna tiktoker maarufu ambaye alikuwa akizikwa leo Kiambu anayeitwa Brian Chira. Tunafariji familia na marafiki," Seneta Cherargei alisema katika seneti.

Mwanasiasa huyo aliendelea kuwashauri vijana kuwa waangalifu na makini na maisha yao na kuepuka kujiingiza katika mambo yanayowaweka hatarini.

"Ninawaomba vijana kuwajibika katika maisha yao, na kuwa makini. Hasa unapoenda kujivinjari  jijini na mijini," alisema.

Seneta huyo alisema hayo wakati marehemu mtayarishaji huyo wa maudhui ya tiktok akizikwa katika eneo la Githunguri, kaunti ya Kiambu.

Mwili wa marehemu ulichukuliwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta Jumanne asubuhi.

Mashabiki, familia na marafiki waliutazama mwili wa TikToker huyo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Waombolezaji walielekea kaunti ya Kiambu kwa mazishi ambayo yalihudhuriwa na TikToker wenza, watu mashuhuri na vyombo vya habari vya mtandaoni.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria maziko hayo ni pamoja na Otile Brown ambaye aliimba wimbo wake maarufu wa 'One Call' na mwanasiasa Peter Salasya.

Akiwahutubia waombolezaji, Otile alisema "Naomba tu kusema asante kwa kuniruhusu kuwa pamoja nanyi hapa. Sikumfahamu Chira lakini kupitia wimbo wangu wa 'One Call' nimeona mapenzi yake."

Chira alifariki asubuhi ya Jumamosi tarehe 16 Machi 2024.

Chira alikuwa mtoto wa marehemu Sofia Wambui Chira, mjukuu wa Esther Njeri na mpwa wa Regina Njoki Chira na marehemu Alice Njoki Chira.

Alikuwa binamu wa Ian Mureithi, Ryan Chira, Stacy Chira na Sofia Njeri.