Linda Okello, polisi wa zamani wa trafiki aliyehamia Marekani ameripotiwa kununua nyumba yake katika taifa hilo na kuwa mmiliki mpya.
Mrembo huyo ambaye picha yake ya urembo akiwa kwenye sare rasmi ya polisi ilimfanya kuwa celeb ghafla, hata hivyo hakufurahishwa na baadhi ya maoni haswa kutoka kwa wanaume ambao wanahusisha urembo wake na ufanisi wake kiuchumi.
Okello alishindwa kulifumbia hilo macho na kuenda kwenye ukurasa wa Facebook wa blogu moja ambayo ilikuwa imeripoti kuhusu hatua yake mpya ya kumiliki nyumba, kisha akaamua kuwajibu watu waliokuwa wakitoa maoni yasiyofurahisha kuhusiana na jinsi aliibukia kuwa mmiliki wa nyumba Marekani.
Alisema kwamba kwa muda, amekuwa akiona watu, haswa wanaume katika mitandao ya kijamii wakihusisha hatua ya mwanamke kununua mali yake na umbile lake, akionekana kuashiria kwamba wengi huhisi wanawake wenye umbile nzuri wanatumia fursa hiyo kujiuza ili kupata mali.
Mrembo huyo maarufu kwa umbile lake kwenye sare ya polisi alisema kwamba dhana kama hizo zinapotosha jamii, haswa katika kizazi kinachokua cha wasichana ambao watadhani kuwa ‘nyash’ ndio kila kitu katika maisha ya mafanikio ya mwanamke.
“Leo nataka kujibu watu wachache hapa! Nataka kunyoosha maelezo kwa sababu nimeona hata wanaume wote wenye watoto hasa wasichana wakizungumzia Nyash, kwa nini tunachochewa au kuwachochea au kuwaharibia wasichana wadogo akili kwamba Nyash inalipa? Nani au nini huamua utajiri au maendeleo ya mtu?” Okello aliuliza.
“Kwa nini jamii huwa na tabia ya kuwadhania vibaya wanawake walio na nyuma inayoonekana kidogo? Je, wale walio na Nyash ya wastani au wasio nayo kabisa wanahisije? wanajitahidi kweli? Kumbuka "sisi" hivi baada ya shule wanawake wenye Nyash kubwa huenda wapi? Kwenye loji?” aliuliza tena.
Okello alisema kuwa jamii ya sasa inatia presha kwa mtoto msichana kumfanya afikirie kwamba akiwa na ‘Nyash’ nzuri basi hahitaji tena kutia bidii maishani ili kujitafutia mali kwa jasho lake halali.
Aidha, aliwataka wanaowachukia wanawake kisa tu kupata mali kwa jasho lao, basi kuanza na wazazi wao wa kike.
“Je, tunajaribu kufundisha nini kizazi kijacho? Kwamba ukiwa na muinuko huo mdogo huhitaji kuendeleza elimu yako au kufanya kazi kwa bidii? Ni watu wangapi wembamba watacheza dansi mtandaoni na kuhukumiwa, je kipande hicho cha nyama kinaleta mabadiliko? Aaaah ukitaka kumchukia mwanamke anza na mama yako na watoto wako kama unaye,” alimaliza kwa hasira.